Mwandishi wa CNN amgomea Trump akiwa Ikulu

Muktasari:

Mwandishi huyo, Jim Acosta alitaka kufahamu hatma ya wahamiaji zaidi ya 4,000, swali lililoonekana kumkera Trump ambaye aliagiza apewe kipaza sauti mwandishi mwingine lakini Acosta alionekana kugoma.

Washington,Marekani. Maofisa wa Ikulu ya Marekani wamemzuia mwandishi wa Kituo cha CNN anayehusika na habari za Ikulu, Jim Acosta kuandika habari za Rais wa Marekani, Donald Trump.

Mwandishi huyo amezuiwa kuandika tena habari zinazomhusu Rais Trump kwa kile walichokisema kwamba amemuuliza Rais swali lisilofaa.

Acosta Juzi alitaka kufahamu hatma ya wahamiaji zaidi ya 4,000 wa Amerika ya Kati ambao wanatembea kupitia Mexico kuomba hifadhi Marekani. Ghafla Rais Trump akamjibu kifupi kwamba ‘’Tunaenda’’

Acosta alipinga matumizi ya maneno ambayo Trump huwa anayatumia kwa wahamiaji hususan neno uvamizi , Trump akamwambia ‘’Unataka waje kwa kuvunja sheria.’’

Wakati Trump alipotaka kumruhusu mwandishi mwingine Acosta alikataa kurudisha kipaza sauti na kuendelea kuuliza maswali mengine.

Akitaka kujua alipofikia  mchunguzi maalumu Robert Mueler kuhusu uchunguzi wa kilichotokea wakati wa kampeni 2016.

Trump hakuweza kujibu swali hilo huku akimtaka kuweka chini kipaza sauti ‘’Weka chini hicho kipaza sauti’’ aliamrisha hapo ndipo wasimamizi wa mkutano wakiwamo maofisa wa Ikulu walipolazimika kumtoa nje lakini akawa anagoma.

"Usikivunjie heshima chombo chako cha habari,’’Trump alisema. "Wewe ni mtu mbaya, mwenye kutisha. Hukupaswa kufanya kazi CNN," alisema Trump.

Tukio hilo lilitokea Jumatano wakati Rais huyo  alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Ikulu ya White House.

Acosta alituma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter Jumatano jioni akisema kwamba Ofisa wa Ikulu aliyemtoa kwenye mkutano hana makosa kwani alikuwa akifanya kazi yake.

"Najua alikuwa akifanya kazi yake, hivyo siyo kosa lake,’’aliandika Acosta

Msimamizi wa mkutano huo Sarah Sanders aliandika kwenye mtandao kwamba mwandishi huyo anatakiwa kuacha mara moja kuandika habari za Ikulu kwa sababu alikataa kurudisha kipaza sauti kama alivyotakiwa.

Alisema mwandishi huyo alikataa kurudisha kipaza sauti kama alivyoamriwa na Rais Trump  huku akimzuia kwa mkono ofisa wa Ikulu  aliyekuwa anatakiwa kuchukua kipaza sauti hicho kama alivyoamriwa.

 "Hii imewachukiza waandishi wengine ambao pia walikuwa wanataka kuuliza maswali’’alisema Sanders

 

Januari mwaka huu

Rais alichukizwa na maswali ya mara kwa mara kuhusu kauli yake ya kuita Mataifa ya Afrika kuwa machafu.

Pia mwishoni hafla ya pamoja na Rais Nursultan Nazarbayev wa Kazakhstan, Trump aliulizwa na Acosta kama alisema katika mkutano wa chama chake  kuwa anapendelea zaidi wageni kutoka Norway .

Pia alimuuliza kwamba anapendelea wahamiaji kutoka nchi za watu weupe au jamii ya kihindi. Trump akajibu nje,

Trump na Acosta pia waliwahi kukwaruzana baada ya kuchapishwa kwa nyaraka kuhusu uhusiano na Russia huku Trump akisema “Nyinyi ni habari za kubuni’’