Uhamiaji yataja sababu za kuwakamata waandishi wa habari wa CPJ

Muktasari:

Idara ya Uhamiaji nchini Tanzania imesema iliwakamata wafanyakazi wa CPJ, Angela Quintal na Muthoki Mumo kwa kukiuka masharti ya viza, kufanya mikutano na wanahabari badala ya matembezi

Dar es Salaam. Idara ya Uhamiaji nchini Tanzania, imetaja sababu ya kuwakamata na kuwashikilia kwa muda waandishi wa habari kutoka Kamati Maalum ya Kuwatetea waandishi wa habari duniani (CPJ).

Pamoja na kuwaachia huru, idara hiyo imesema inaendelea kushikilia hati zao za kusafiria kwa uchunguzi zaidi.

Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Novemba 8, 2018 Msemaji wa Idara ya Uhamiaji, Ally Mtanda amesema, ‘’ni kweli idara yetu iliwakamata waandishi hao katika maeneo ya hoteli waliyofikia na kufanya nao mahojiano, kwa sababu tulifanya uchunguzi na kubaini wanaenda kinyume na masharti yaliyoainishwa katika madhumuni ya ujio wao hapa nchini.”

Mtanda amesema, waandishi hao Angela Quintal na Muthoki Mumo waliingia nchini Oktoba 31, 2018 kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar na katika madhumuni ya safari yao walisema wanaingia nchini kwa matembezi ya kawaida na viza yao ilikuwa inafikia ukomo Januari 1, 2019.

Amesema lakini baadaye maofisa wetu katika uchunguzi, walibaini wafanyakazi hao wa CPJ wanafanya mikutano na waandishi wa habari, jambo ambalo ni kinyume na madhumuni waliyoyataja hapo awali.

“Idara yetu haiishii tu kwenye kutoa viza, bali huwa tunafuatilia kama muhusika anafuata masharti aliyopewa katika viza, kwa kuendana na madhumuni aliyoyaainisha awali ya kuingia nchini,” amesema Mtanda

Mtanda amesema baada ya kuwashikilia kwa muda, tuliwaelekeza na kuwafundisha nini wanapaswa kufanya kuendana na masharti ya viza yao, kwa sababu kama walikuwa na lengo la kufanya mikutano na waandishi wa habari, basi walipaswa kuwasiliana na Idara ya Habari Maelezo na mamlaka zinazohusika kabla ya kuanza kufanya shughuli hizo.

“Baada ya kuwashikilia na kuwaelimisha, tuliwaachia jana Jumatano hiyo hiyo na tuliendelea kushikilia hati zao za kusafiria na tunafanya mchakato wa kuwarudishia,’’ amesema Mtanda.