Wateja Halopesa kuanza kulipa kwa msimbo wa QR

Muktasari:

Kampuni ya Halotel imeungana na Visa kuwaruhusu wateja wa Halopesa kutumia huduma za mfumo wa msimbo wa QR ili kufanya malipo ya kimataifa.

Dar es Salaam. Wateja wa Halopesa wataanza kufanya malipo kwa kutumia mfumo wa msimbo wa QR (QR code) baada ya kampuni ya Halotel kuingia mkataba wa kufanikisha hilo na kampuni ya Visa.

Huduma hiyo itaanza kupatikana mwanzoni mwa mwaka 2019 kuwezesha zaidi ya wateja milioni moja  wa Halopesa kufanya malipo ya biashara kwa njia salama na ya uhakika pamoja na kuweka au kutoa fedha kwa mawakala wa Visa.  

Meneja mkuu wa Visa, ukanda wa Afrika Mashariki, Kevin Langley amesema mteja wa Halopesa, hata wale ambao hawana akaunti ya benki, wataweza kufaidika na mfumo huo wa malipo ya kimataifa.

"Ushirikiano wetu na Halotel utahakikisha Watanzania wanaweza kufanya malipo ya QR Visa kwa wauzaji  na wafanyabiashara zaidi ya 40,000 waliopo nchini kwa kutumia simu zao za mkononi,” anasema Langley.

Taarifa iliyotolewa leo, Novemba 8 na kampuni ya Visa inasema zaidi ya wateja milioni nne wa Halotel wanaweza kutumia fursa hiyo kufanikisha malipo ya kimataifa.

Naibu mkurugenzi wa Halotel, Nguyen Van Son amesema fursa hiyo inawahusu wateja waliopo na watakaojiunga na mtandao huo huko mbeleni.

Ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuhusu Halotel iliyoanzishwa mwaka 2015, inaonyesha hadi Juni, kampuni hiyo ilikuwa inahudumia zaidi ya wateja milioni 3.65 wakiwamo zaidi ya 750,000 wanaotumia Halopesa.