VIDEO: 43,200 wafanyiwa upasuaji Moi tangu mwaka 2015

Friday November 22 2019

By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Taasisi ya Mifupa (Moi) imesema kuanzia mwaka 2015 imewafanyia upasuaji wagonjwa 43,200 huku asilimia 10 wakiwa ni raia kutoka nje na asilimia 40 waliopata ajali.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa Novemba 22, 2019 na mkurugenzi mtendaji wa taasisi hiyo, Dk Respicious Boniface wakati akitoa taarifa ya mafanikio ya miaka minne ya taasisi hiyo ya afya tangu Rais John Magufuli alipoapishwa kuwa kiongozi mkuu wa nchi Novemba 5, 2015.

Dk Respicious amesema uboreshaji uliofanyika umesaidia Moi kuendelea kuboresha matibabu ya mifupa, ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu na kuongeza idadi ya wagonjwa wa upasuaji kutoka 400 hadi  500 kwa mwezi hadi 700 mpaka 900 kwa mwezi.

“Katika kipindi hicho wagonjwa 43,200 wamefanyiwa upasuaji ikiwemo kubadilisha nyonga ambao walikuwa  900. Kubadili magoti 870, upasuaji wa mfupa wa kiuno 618, upasuaji wa ubongo 880, watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi 2,070,” amesema.

Amesema gharama za matibabu hayo ndani ya nchi ilikuwa Sh16.5 bilioni, “kama wangepelekwa nje ya nchi kwa matibabu Sh54.9 bilioni zingetumika, taasisi imeokoa Sh38.4 bilioni ambazo zitatumika kwa shughuli nyingine za maendeleo ya nchi.”

Advertisement