AIC Tanzania kutumia Jumapili ya Agosti 18 kuombea majeruhi wa ajali ya moto Morogoro

Wednesday August 14 2019

 

By Rehema Matowo, Mwananchi [email protected]

Geita. Askofu mkuu wa Kanisa la African Inland Church (AIC) Tanzania, Musa Magwesela amewataka wachungaji na waumini wa kanisa hilo kote nchini, kuitumia Ibada ya Jumapili Agosti 18, 2019 kuwa siku maalumu ya maombi kwa ajili ya kuwaombea majeruhi na familia zilizopoteza wapendwa wao katika ajali ya moto iliyotokea  Agosti 10,2019 eneo la Msamvu mkoani Morogoro

Akizungumza wakati wa kufungua semina ya wachungaji wa kanisa hilo mkoani Geita leo Jumatano Agosti 14, 2019, Askofu Magwesela amewataka wachungaji kutumia Ibada ya Jumapili kuonyesha matendo ya huruma kwa familia zilizopatwa na majanga.

Mbali na kutenga Ibada maalumu ya kuwaombea majeruhi na familia zilizopoteza ndugu zao, Askofu Magwesela amewataka waumini wa kanisa hilo kutenga siku hiyo pia kuchangia damu kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa katika hospitali mbalimbali nchini.

Aidha, amewasihi viongozi wa dini nchini kuwatembelea majeruhi na kuwatia moyo hospitalini pamoja na kuzitembelea familia zilizopoteza wapendwa wao na kuzifariji kwa kutoa ushauri wa kisaikolojia .

“Tuwatembelee wenzetu tuwashauri tuwatie moyo lakini tuwaombee watoa huduma madaktari na wauguzi ili tiba wanazotoa ziwasaidie na kuwaponya majeruhi,” amesema Askofu Magwesera

Naye Mchungaji Obed Kulu wa kanisa hilo, ameitaka jamii kujifunza kutokana na tukio la moto lililotokea Morogoro na kuwataka wananchi kuweka utu mbele pindi mtu anapopatwa na tatizo badala ya kutumia tatizo lake kama fursa ya kujipatia mali isiyo halali.

Advertisement

Ajali ya moto iliyotokea eneo la Msamvu mkoani Morogoro Agosti 10, 2019 imesababisha vifo vya watu zaidi ya 80 na majeruhi.

Advertisement