Acacia, UDSM kusomesha wataalamu wa madini

Kampuni ya Acacia imeingia makubaliano ya kuwajengea uwezo watalaamu wa madini nchini baada ya kusaini makubaliano na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

 

BY Aurea Simtowe, Mwananchi asimtowe@mwananchi.co.tz

IN SUMMARY

  • Katika utekelezaji wa makubaliano hayo yaliyoingiwa jana, kampuni hiyo inayoongoza kwa uchimbaji wa dhahabu itakuwa inawafadhili wanafunzi na walimu wa chuo kikuu hicho kuhakikisha maarifa yanayohitajika kwenye uchimbaji yanakuwapo.

Advertisement

Dar es Salaam. Kampuni ya Acacia imeingia makubaliano ya kuwajengea uwezo watalaamu wa madini nchini baada ya kusaini makubaliano na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Katika utekelezaji wa makubaliano hayo yaliyoingiwa jana, kampuni hiyo inayoongoza kwa uchimbaji wa dhahabu itakuwa inawafadhili wanafunzi na walimu wa chuo kikuu hicho kuhakikisha maarifa yanayohitajika kwenye uchimbaji yanakuwapo.

Kwenye utiaji saini wa makubaliano hayo, Acacia imetoa ufadhili wa masomo kwa mwalimu Dismas Kalitenge ambaye atakwenda kusoma shahada ya uzamili ya uhandisi wa madini nchini Canada katika Chuo Kikuu cha Alberta.

Akizungumza katika mkutano wa kusaini mkataba huo, mkurugenzi mtendaji wa Acacia, Asa Mwaipopo alisema mbali na ufadhili huwa wanatoa nafasi ya kufanya mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa uhandisi wa madini katika migodi yao ili kuwaongezea ujuzi.

"Ni kwa mara ya kwanza Acacia tunatoa ufadhili. Tunafikiri tumefungua milango ya kufanya hivi kwa watu wengine kusaidia kujenga jukwaa la maendeleo," alisema Mwaipopo.

Ufadhili uliotolewa ni wa jumla ya Dola 60,000 za Marekani (sawa na Sh137 milioni) ikiwa ni hatua ya kuboresha na kuongeza wataalamu wa fani hiyo.

Alisema kunapokuwa na wanafunzi bora inakuwa chachu kwa waajiri kujihakikishia kupata wafanyakazi wenye sifa nchini bila kufikiria kuwatafuta nje na kwa kuwa wanafanya mafunzo kwa vitendo kwao inakuwa rahisi pia kuwachuja kabla ya kuwaajiri.

"Asilimia 70 ya wanafunzi wa fani ya uhandisi wa madini UDSM wa mwaka wa pili na wa tatu huwa wanafanya mafunzo katika migodi ya Buzwagi, North Mara na Bulyanhulu," alisema.

Makamu mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye amesema ufadhili huo ni muhimu kuendeleza rasilimali watu chuoni hapo hasa maeneo ambayo yana uhitaji mkubwa.

"Tunaamini atakaporudi atakuwa msaada katika kusimamia utafiti kwa wanafunzi na kuwapa ujuzi wa kile alichokipata katika nchi za wenzetu," alisema Profesa Anangisye.

Kwa upande wake Kalitenge amesema ana deni kubwa kwa sababu anapaswa kuhakikisha ujuzi atakaoupata Canada unazaa matunda si ndani ya chuo tu bali kwa Taifa pia.

"Nitarudi kuhakikisha nilichotumwa matunda yake yanaonekana na kuleta faida kwa kila mtu anayenizunguka," amesema Kalitenge.

More From Mwananchi
This page might use cookies if your analytics vendor requires them. Accept