Ahsante Mzee Majuto

Muktasari:

  • Mzee Majuto ambaye amehitimisha safari yake hapa duniani juzi, alitumia zaidi ya miaka 40 kuwachekesha Watanzania katika majukwaa, sebule na vyombo vya usafiri.

Neno ‘Ahsante’ ndilo pekee analostahili kuambiwa mfalme wa vichekesho nchini, Amri Athuman maarufu Mzee Majuto. Mwonekano wa sura yake tu vilitosha kuijaza tabasamu sura yako na vichekesho vyake viliwavunja mbavu za Watanzania kwa miaka mingi. Kama ucheshi unatibu maradhi, basi Mzee Majuto ameponya wengi.

Mzee Majuto ambaye amehitimisha safari yake hapa duniani juzi, alitumia zaidi ya miaka 40 kuwachekesha Watanzania katika majukwaa, sebule na vyombo vya usafiri.

Unawezaje kupanda mabasi yanayokwenda masafa marefu na usifurahie safari yako zinapowekwa filamu alizocheza Mzee Majuto?

Kabla ya umauti, alizushiwa kifo mara kadhaa na kauli yake ya mwisho alipozungumza na mwandishi wetu, Rhobi Chacha Juni 22 alizungumzia hilo akisema, “Mwambieni huyo anayetaka nife bado napumua, asiniharakishe safari yangu bado haijafika.”

Mbali na kuchekesha, Mzee Majuto amechangia mabadiliko kwenye tasnia ya sanaa nchini kwa kuibua vipaji na kuwa mfano wa kuigwa kwa kuishi maisha ya kawaida yasiyotawaliwa na kashfa kama ilivyo kwa baadhi ya wasanii wenye majina makubwa nchini.

Filamu za kuvunja mbavu alizocheza kama Sharobaro, Gumzo, Nakwenda kwa Mwanangu, Inye Gwedegwede, Mzee wa Chabo, Daladala, Swaga, Nyumba Nne na Mshamba, ni kielelezo cha mchango wake katika kuichekesha Tanzania.

Baada ya kupokea taarifa za msiba huo jana, Waziri wa Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe aliandika katika ukurasa wake wa Instagram: “Ahsante King Majuto kwa kuitendea haki tasnia ya filamu, kwa kuwapa burudani mamilioni ya wapenda filamu nchini na nje ya nchi na kwa kutufundisha wanadamu thawabu ya kicheko kupitia maigizo yako na tabasamu lililokuwa usoni kwako daima. Mwenyezi Mungu aiweke roho yako pema peponi. Amina.”

Mwanamuziki Ambene Yessaya maarufu AY pia amendika katika ukurasa wake wa Instagram: “Ahsante sana kwa kushare na sisi kipaji chako hakika tulikufurahia tangu wengine tukiwa watoto.”

Mwaka mmoja wa kuugua

Kwa zaidi ya mwaka mmoja jina la Mzee Majuto lilitawala vyombo vya habari likihusishwa na ugonjwa wa henia na baadaye tezi dume.

Taarifa za kuugua kwake ziliripotiwa Julai mwaka jana na mkewe Aisha Yusuf ambaye alisema marehemu Mzee Majuto alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa huo tangu Mei.

Januari, Mzee Majuto ambaye pia alijulikana kwa jina la King Majuto alifanyiwa upasuaji wa tezi dume katika Hospitali ya Tumaini jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, kidonda cha upasuaji wa henia kiliendelea kumsumbua na alilazwa kwa mara nyingine katika hospitali hiyo katikati ya Aprili.

Serikali iliamua kumpeleka India Mei 4 kwa matibabu zaidi katika Hospitali ya Apollo, New Delhi na alirejea Juni 23 na moja kwa moja alipelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya uangalizi kabla ya kuruhusiwa na kisha kurudishwa tena hospitalini hapo Julai 31 ambako alilazwa hadi kifo chake.

Mamia wamuaga

Jana, Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu Abubakary Zubeiry aliongoza dua ya kumuombea marehemu katika Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam kabla ya mwili wa marehemu kusafirishwa kwenda Tanga kwa mazishi leo.

Rais John Magufuli aliongoza mamia ya waombolezaji waliojitokeza kumuaga msanii huyo mkongwe katika ukumbi huo. Wengine waliohudhuria ni Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, Dk Mwakyembe na naibu wake, Juliana Shonza, mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salum, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Joyce Fisoo.

Mbali ya viongozi hao na wengine, pia walikuwapo wasanii wa fani mbalimbali akiwamo Diamond Platnumz, Nisha, Steve Nyerere, Cloud 112 pamoja na ndugu jamaa na marafiki.

Kabla ya kupelekwa Karimjee, mwili wake uliswaliwa katika msikiti wa Maamur, Upanga Dar es Salaam.

Tanga yazizima

Jijini Tanga, vilio na simanzi vilitawala nyumbani kwa msanii huyo mkongwe Afrika Mashariki katika Mtaa wa Donge pamoja na Kijijini kwake Kiruku, Kata ya Mabokweni wilayani Tanga.

Waandishi wetu walifika nyumbani kwa marehemu Donge na kijijini Kiruku na kukuta watu wakiwa wamekusanyika kuomboleza msiba huo.

Mwenyekiti wa kamati ya mazishi, Hassan Hashim alisema mwili wa marehemu King Majuto unatarajiwa kupokewa jijini Tanga kati ya saa 3.00 hadi saa 4.00 usiku na leo shughuli za kuuaga na kuswalia zitaendelea hadi mchana utakapopelekwa Kiruku kwa mazishi.

Wasifu wa Mzee Majuto

King Majuto aliyeacha mjane, watoto 10 na wajukuu 19, alizaliwa mwaka 1948 huko Mwang’ombe, Tanga na kupata elimu katika shule za Msambweni na Changa zote zikiwa za Tanga.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kiruku, Omary Mwasumba alisema wameanza kusafisha eneo ambalo Mzee Majuto wakati wa uhai wake aliomba kuzikwa baada ya kifo chake.

“Hapa kwetu ni majonzi makubwa kwa sababu, King Majuto alikuwa mwenzetu na msaada mkubwa katika kijiji hiki, amejenga msikiti na alikuwa akijitolea misaada mbalimbali tukifiwa na hata kwenye masuala ya sherehe kama Idd,” alisema Mwasumba.

Kaimu katibu tawala Wilaya ya Tanga ambaye pia ni ofisa Tarafa ya Ngamiani, Tanga, Suleyman Zumo alisema Serikali inashirikiana na familia ya King Majuto kuratibu shughuli za msiba huo kuanzia nyumbani kwake Donge hadi Kiruku atakakozikwa leo.

Aacha wasia mzito kwa familia

Akizungumza nyumbani kwao Donge, mmoja wa watoto wa marehemu, Mohammed Amri alisema baba yao aliwausia kuwa wamoja na kuzingatia dini.

Mohammed alisema siku chache kabla ya kifo, Mzee Majuto alimwambia ili afurahi, angependa kuwaona watoto wake wakipendana na kushikamana katika hali zote.

“Baba akiwa kitandani aliniambia ‘mwanangu nitafurahi sana kama mtashikamana na ndugu zako na mkifuata misingi ya dini,” alisema.

Akiwa msaidizi wa kikundi cha marehemu baba yake cha King Majuto Cultural Group, Mohammed alisema mbali na kufuata yale aliyoagizwa na baba yake, atamuenzi kwa kuendeleza sanaa ya maigizo kitu ambacho alipenda.

“Nitamuenzi baba kwa kuliendeleza kundi lake ambalo aliniamini tangu mwanzo kulisimamia, pia nitafuata yale aliyoniusia siku chache kabla ya kufariki dunia,” alisema Mohammed.