Airtel Money kujaza noti wateja

Dar es Salaam. Ili kuhamasisha utunzaji wa fedha, kampuni ya Airtel imetangaza kuanza kutoa asilimia tano kwenye akiba itakayokuwapo kwenye akaunti ya kila mteja kila mwezi, hivyo kuwawezesha wateja wake kuwa na chanzo kipya cha mapato.

 

BY Julius Mnganga, Mwananchi mathias@mwananchi.co.tz

Advertisement

Dar es Salaam. Ili kuhamasisha utunzaji wa fedha, kampuni ya Airtel imetangaza kuanza kutoa asilimia tano kwenye akiba itakayokuwapo kwenye akaunti ya kila mteja kila mwezi, hivyo kuwawezesha wateja wake kuwa na chanzo kipya cha mapato.

Katika huduma hiyo inayoitwa ‘Timiza Akiba’, Airtel imesema itatoa riba hiyo kwa wateja watakaokuwa na salio la kuanzia Sh100 hadi Sh4 milioni kwenye akaunti zao za Airtel Money bila kutoa ndani ya mwezi mmoja.

Mkurugenzi wa masoko wa Airtel Money, Isack Nchunda alisema jana kuwa hiyo ni huduma rahisi, isiyo na makato itakayompa mteja zawadi ya fedha kila mwezi kwa kujiwekea akiba binafsi ili kutimiza malengo.

“Tunaamini huduma hii itawawezesha kujiwekea akiba zao kwa uhakika zaidi. Tulikusudia kuifanya iwe huduma rahisi ili kuwanufaisha watu wengi kutumia huduma za fedha zinazokidhi mahitaji yao,” alisema.

Kwa hatua hiyo, mteja ana uhakika wa kupata Sh50,000 kwa mwezi akiweka Sh1 milioni au Sh100,000 akitunza Sh2 milioni au Sh150,000 akihifadhi Sh3 milioni na Sh200,000 endapo ataweka Sh4 milioni ambacho ni kiwango cha juu.

Nchunda alisema akaunti ya Timiza Akiba inaendeshwa kwa ushirikiano na Benki ya Letshego na kampuni ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ya Jumo.

“Timiza Akiba inawapa Watanzania fursa ya kukuza akiba itakayosaidia kukabiliana na dharura na majanga yasiyotarajiwa kwa siku za baadaye endapo yatajitokeza,” alisema.

Akizungumzia hatua hiyo ya Airtel, mhadhiri mwandamizi wa Chuo cha Biashara (CBE), Dk Dickson Pastory alisema itaiongezea pamoja na Benki ya Letshego ambayo itakuza kiasi cha amana inazopokea. Hata hivyo, alionyesha wasiwasi wake kama itakuwa endelevu.

“Hii ni riba kubwa sana. Inahamasisha kwa sababu kama mteja ataziacha fedha zake mwaka mzima atakuwa na uhakika wa kupata asilimia 60. Ukiweka Sh4 milioni baada ya mwaka unapata faida ya Sh2.4 milioni hivyo jumla ni Sh6.4 milioni,” alisema.

Mtaalamu wa masuala ya benki na mikopo, Reginald Baynit alisema huenda riba waliyoitangaza ni ya mwaka mzima, ila malipo ndiyo yatafanyika kila mwezi.

“Wateja wakifahamu masharti yaliyopo, wapo watakaotoa fedha zao kwenye miradi mingine na kuziwekeza huko. Siamini kama riba hiyo ni ya mwezi. Itakuwa ni mwaka mzima,” alisema Baynit.

“Riba hizo ni kwa mwaka, siyo mwezi mmoja kama watakavyofanya Airtel. Wataweza kutoa riba hiyo endapo watakuwa na uhakika wa kukopesha fedha hizo kwa riba isiyopungua asilimia nane,” alisema.

More From Mwananchi
This page might use cookies if your analytics vendor requires them. Accept