Ajali yawapeleka mawaziri Mbeya

Siku mbili baada ya kutokea kwa ajali iliyosababisha vifo vya watu 15 na majeruhi 15 jijini Mbeya Ijumaa iliyopita, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Yusuph Massauni ameagiza kukamatwa kwa mmiliki wa Lori lililosababisha ajali na ili athibitishe kama gari lake lilistahili kuwapo barabarani na kama dereva wake alikuwa na ujuzi unaokubalika kisheria kuendesha gari.

 

BY Godfrey Kahango, Mwananchi gkahango@mwananchi.co.tz

IN SUMMARY

  • Ajali hiyo ilitokea katika eneo la Mlima Igawilo ikihusisha magari matano yote yakitokea barabara ya Tukuyu kwenda Jijini Mbeya.

Advertisement

Mbeya. Siku mbili baada ya kutokea kwa ajali iliyosababisha vifo vya watu 15 na majeruhi 15 jijini Mbeya Ijumaa iliyopita, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Yusuph Massauni ameagiza kukamatwa kwa mmiliki wa Lori lililosababisha ajali na ili athibitishe kama gari lake lilistahili kuwapo barabarani na kama dereva wake alikuwa na ujuzi unaokubalika kisheria kuendesha gari.

Ajali hiyo ilitokea katika eneo la Mlima Igawilo ikihusisha magari matano yote yakitokea barabara ya Tukuyu kwenda Jijini Mbeya.

Chanzo cha ajali hiyo ni lori moja lililokuwa limebeba viazi kudaiwa kufeli breki kisha kuligonga gari la abiria lililokuwa likitokea Igoma kwenda Mbeya mjini na kisha kuyagonga magari mengine matatu, mawili kati ya hayo yalikuwa yamebeba mafuta na moja lilikuwa limebeba ndizi. Gari moja liliwaka moto.

Jana, Masauni akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Miundombinu, Elias Kwandikwa na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus Muslimu walifika eneo la tukio.

“Nataka huyu mmiliki wa gari hili lililosababisha ajali akamatwe mara moja aweze kututhibitishia mambo mawili, kwanza atueleze kama gari hili halikuwa bovu kabla ya kupata ajali na pili atueleze kama dereva wake huyo alikuwa mzima na mwenye ujuzi unaokubalika kisheria kuendesha gari,” alisema Masauni.

Alisema Sheria ya Usalama Barabarani inaelekeza kila mmiliki wa chombo cha moto kuhakikisha gari lake linaendeshwa likiwa zima, hivyo kama lilikuwa bovu ni kosa kwa mujibu wa sheria.

Kwandikwa alisema barabara hiyo na nyingine za Mkoa wa Mbeya zina miteremko mirefu inayochukua muda mwingi kuipita hivyo kuna haja ya kuzipanua ili kuepusha ajali. Alisema upo umuhimu wa kuchukua hatua kupunguza makosa ya kibinadamu barabarani ambayo alisema kwa kiwango kikubwa ndiyo yanayosababisha ajali.

Alisema ‘Kutokana na ukuaji wa uchumi na maendeleo huku kukiwa na ongezeko la magari mkoani Mbeya na changamoto ya barabara kuwa katika miteremko mirefu na mikali, kuna haja pia kwa Serikali kuangalia uwezekano wa kuzipanua hususani maeneo ya milima ili kupunguza magari kusogeleana yakiwa milimani.

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus Muslimu, mbali na kuahidi kutekeleza agizo la Serikali la kumkamata na kumchukulia hatua za kisheria mmiliki wa lori hilo, alisema nia ya Jeshi la Polisi ni kuhakikisha wanabaki na madereva wenye sifa barabarani.

Alisema jeshi hilo limebaini kuendesha gari sio tatizo kwa madereva wengi, isipokuwa yapo mambo matano ambayo wanahitaji kuelimishwa zaidi ili kuepuka ajali.

Aliyataja mambo hayo kuwa ni kuwafundisha madereva udereva wa kujihami, sheria za usalama barabani, utambuzi wa alama za bararani, utambuzi wa hali ya barabara na matumizi sahihi ya gia za magari kulingana na maeneo waliyopo wawapo barabarani.

More From Mwananchi
This page might use cookies if your analytics vendor requires them. Accept