Albamu ya Vanessa Mdee kuinufaisha familia ya Mbaraka Mwishehe

Muktasari:

Mdee aliyasema hayo jana Ijumaa kupitia ukurasa wake wa Instagram, ikiwa ni muda mfupi tangu alipokwenda kuitembelea familia hiyo kwa ajili ya kupata ridhaa yao

Wakati leo Jumamosi akitarajia kuanza kuuza CD ya albamu yake ya ‘MondayMondays’ pale Mlimani City jijini Dar es Salaam, msanii wa muziki wa kizazi kipya, Vanessa Mdee amesema wimbo wa Pumzi ya mwisho nusu ya mauzo yake yatakwenda kwa  familia ya mwanamuziki marehemu Mbaraka Mwinshehe.

Mdee aliyasema hayo jana Ijumaa kupitia ukurasa wake wa Instagram, ikiwa ni muda mfupi tangu alipokwenda kuitembelea familia hiyo kwa ajili ya kupata ridhaa yao.

Amesema wimbo huo ni  moja ya nyimbo anazozipenda kwenye albamu yake hiyo ni kati ya nyimbo zake bora na sababu ya kuichagua ni kutokana na midundo yake kuwa na  kionjo kimoja kutoka kwenye wimbo wa hayati Mbaraka Mwinshehe.

“Kabla ya album kutoka nikaona ni vema kuwaona familia ya Mbaraka kwanza ili nipate idhini ya kuendelea na kazi hiyo na kuona watanufaika vipi kama familia kupitika huo wimbo.

“Nashukuru walinipokea vizuri sana na walitoa idhini yao kwa mikono miwili kabisa hivyo nusu ya mauzo ya wimbo huu kwenye mitandao ya kidijitali yataenda kwenye familia ya mzee huyu siku zote,” ameandika V Money.