Alichokisema bilionea wa Tanzania Mo Dewji mitandaoni

Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’.

What you need to know:

  • Kama ilivyo kwa watu wengine mfanyabiashara Mohammed Dewji pia ni mtumiaji mzuri wa mitandao ya kijamii, siku kadhaa kabla ya kutekwa alitumia mitandao hiyo kuandika ujumbe mbalimbali, hasa akilenga kuwatia moyo waliokata tamaa.


Dar es Salaam. Tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara maarufu nchini Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ ambaye ni mshindi wa zabuni ya kuwekeza kwenye klabu ya Simba kwa kiwango cha hisa asilimia 49 limetikisa kila kona.

Mfanyabiashara huyo alitekwa jana alfajiri Oktoba 11, 2018 jijini Dar es Salaam kwenye Hoteli ya Colosseum iliyopo Oysterbay alipokwenda kwa lengo la kufanya mazoezi.

Kama ilivyo kwa watu wengine, Dewji ni mpenzi wa mitandao ya kijamii, amekuwa akiitumia kuandika ujumbe mbalimbali unaochangiwa na watu wa kada mbalimbali.

Siku 10 kabla ya kutekwa, bilionea huyo kijana alitumia kurasa za mitandao yake ya kijamii kutuma ujumbe mbalimbali.

Ujumbe alioutuma kwenye Ukurasa wake wa Twitter, Oktoba 10, 2018  ulisomeka hivi kwa lugha ya Kiingereza, 

"Why aren’t schools teaching students how to do taxes and personal budgeting?

Kwa kiswahili alimaanisha; Kwa nini wanafunzi mashuleni hawafundishwi kuhusu kodi na kujiwekea bajeti?

Siku hiyohiyo aliandika ujumbe mwingine, "Your ability to handle chaos determines how you progress in life. How you manage and embrace chaos will always be one of your greatest strengths."

Akimaanisha; Uwezo wako wa kukabiliana na usumbufu, ni kipimo cha namna unavyopiga hatua kwenye maisha. Jinsi unavyodhibiti na kuondoa usumbufu ndio kutafanya uwe moja ya uimara wako mkubwa."

Ijumaa Oktoba 5, 2018 mfanyabiashara huyo aliandika,"Kila jambo unaloogopa Mungu ana mpango wake. Mungu ni mkuu kuliko hofu uliyonayo. Ana mamlaka na maisha yako ya baadaye. Kuwa na imani. #JumaahKareem."

Mbali na ujumbe huo, Septemba 26, 2018 aliandika," Hamna kitu kinaua urafiki kama mikopo!

Siku mbili baadaye aliandika ujumbe unaosomeka," The jealous one is always sick, even when his body is healthy.” akinukuu kutoka kwa Swahaba wa Mtume Muhammad (S.A.W), Imam Ali ambapo kwa Kiswahili alimaanisha," mtu mwenye wivu siku zote ni mgonjwa hata kama mwili wake una afya."

Septemba 19, 2018 aliandika," Vitu vingi katika maisha vinaweza kujaribu kukuondoa kwenye malengo yako lakini usipoteze mwelekeo. Mipango inaweza kubadilika lakini kamwe sio mwisho wa safari!

Pia siku hiyo aliandika," “Pride and arrogance are the mother of all evils” Let’s pray to the Almighty GOD to make us stay away form these bad characters."

Alimaanisha; ufahari na ubinafsi ni mama wa mabaya yote. Tumuombe Mungu atuweke mbali na tabia hizo mbaya".

Mwingine ni ule alioandika Septemba 20, 2018  akimnukuu Imam Hussain ibn Ali unaosema, "Truth has only a few friends." Akimaanisha ukweli una marafiki wachache.

Mbali na hizo, hivi karibu alikuwa akituma jumbe za mfululizo za kuonyesha furaha aliyonayo kwa kuanza kwa mchakato wa ujenzi wa Uwanja wa Simba huko Bunju.

Mfano wa jumbe hizo ni ule wa Oktoba 3, 2018;  Kwa miaka mingi nimekuwa nikiota na sisi tuwe na uwanja wetu wa mazoezi, na ninafurahi sasa ninawezesha ndoto hii baada ya miaka 82 tangu kuanzishwa kwa klabu ya Simba. Nimeanza kukamilisha ahadi ya uwanja wa Bunju. Insha Allah kazi ya ujenzi itakamilika kabla ya mwezi wa 2, 2019