Aliyemtukana Rais Museveni apandishwa kizimbani

Muktasari:

Pia mwanasheria huyo anadaiwa kumtukana mama mzazi wa Rais Yoweri Museveni kupitia mtandao wa kijamii

Kampala, Uganda. Msomi na mwanaharakati maarufu wa haki za wanawake nchini Uganda, Stella Nyanzi amefikishwa mahakamani kwa kosa la kumtukana Rais wa Uganda, Yoweri Museveni.

Nyanzi ambaye alikamatwa mwishoni mwa wiki iliyopita ameshtakiwa kwa matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii pamoja na kusambaza maandishi yaliyolenga kushusha hadhi ya Rais Museveni pamoja na mama yake.

Mawakili wake wamekuwa wakilalamikia hatua ya polisi kuendelea kumshikilia  zaidi ya saa 48 zinazohitajika kisheria.

Mmoja wa mawakili wake Issac Semakade amesema mteja wake amesomewa mashtaka yanayomkabili na anatarajiwa kufikishwa tena mahakamani Novemba 9.

Msemaji wa Polisi Uganda, Vincent Sekati aliliambia Shirika la Habari BBC kuwa Stela alikamatwa kutokana na maelezo aliyoyatoa kwenye mtandao wake akimtukana Rais.

Anasema wala hakuishia hapo bali aliendelea mbele na kumtukana mama mzazi wa Rais, “Ni maneno ambayo nisingependa kuyarudia kwa sababu yalikua machafu sana.”

Tukio hilo lilitokea Sepemba 16 mwaka huu na msemaji wa polisi amesema mtu yeyote anaweza kutembelea ukurasa huo kujionea mwenyewe maneno aliyoandika mwanaharakati huyo ikiwa mtandao huo haujafungwa.