Anayedaiwa kumuua mwanafunzi wa chuo akamatwa

Wednesday June 19 2019

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, alipokuwa akitoa taarifa kuhusu kukamatwa kwa mtuhumiwa wa mauaji ya mwananfunzi wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala, Anifa Mgaya. Picha na Ericky Boniphace 

By Bakari Kiango, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema jeshi hilo linamshikilia mtu mmoja akidaiwa kumuua kwa kumchoma kisu maeneo ya kifuani Anifa Mgaya (21), aliyekuwa akisoma Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala (KIU) tawi la Tanzania.

Juni 16, 2019 saa 3 usiku Anifa anadaiwa kuchomwa kisu upande wa kulia wa kifua chake na mtu huyo jina limehifadhiwa wakati akitoka kujisomea katika chuo hicho kilichopo GongolaMboto kisha kuporwa pochi iliyokuwa na simu na fedha Sh8,000.

"Baada ya kumhoji mshtakiwa amekiri kuhusika na tukio hilo, huku akieleza namna ambavyo mwanafunzi huyo wa mwaka pili (ngazi ya Stashahada ya Maabara) alivyokuwa amevaa siku hiyo," amesema Kamanda Mambosasa.

Mwili wa Anifa aliagwa jana Jumanne nyumbani kwao Salasala jijini Dar es Salaam kisha kusafirishwa kwenda Makambako mkoani Iringa kwa mazishi yanayotarajiwa kufanyika kesho Alhamisi.

Katika hatua nyingine, Kamanda Mambosasa amesema polisi linawashirikia watu 31 wanaodaiwa kujihusisha na vitendo vya kihalifu kwenye maeneo yanayopakana na vyuo vikuu katika jiji hilo na uchunguzi zaidi unaendelea.

Advertisement