Apigwa risasi, afariki kwa kukaidi amri ya JWTZ

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Pwani Wankyo Ngigesa akitoa taarifa ya tukio la mtu mmoja ambaye jina lake halijafahamika kuingia ndani ya eneo la  Jeshi la wananchi JWTZ  Mapinga Bagamaoyo kwa kuruka ukuta usiku  na kwamba alipotakiwa kusimama alikaidi amri na kuanza kukimbia hivyo kuwalazimu askari waliokua lindo muda huo kumpiga risasi iliyompata kiunoni na baadae alifariki akipelekwa hospitalini kwa matibabu.

Muktasari:

Mtu huyo alifariki kwa kupigwa risasi ya kiuno baada ya kukaidi amri ya wanajeshi hali iliyosababisha kumpiga risasi iliyompata kiunoni.

Bagamoyo. Mkazi wa Bagamoyo ambaye jina halikutajwa amefariki baada ya kupigwa risasi akidaiwa kukaidi amri ya wanajeshi wakati akiingia kambi ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ)  Bagamoyo, mkoani Pwani.

Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo Septemba 11, 2018 kwenye kambi ya JWTZ Mapinga Comprehensive Training Centre (CTC) kata ya Mapinga wilayani humo.

Kamanda wa polisi mkoani Pwani, Wankyo Nyigesa amekiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba mtu huyu alipigwa risasi baada ya kuingia ndani ya kambi hiyo kwa kuruka ukuta usiku huo.

“Wakati anaruka alionekana na walinzi wa JWTZ waliokuwa zamu muda huo na walimuamuru asimame lakini alikaidi na kuanza kukimbia,” amesema  Nyigesa na kuongeza:

"Askari waliendelea kumsisitiza asimame lakini hakutii hivyo walilazimika kumsisitiza tena kwa kupiga risasi moja hewani, lakini hakuitii aliendelea kukimbilia walipo askari hivyo mmoja wa walinzi alimfyatulia risasi iliyompata kiunoni na kuanguka chini, "

Ameongeza kuwa baada ya kudondoka walimpekua lakini hakukutwa na silaha hivyo jitihada za kumpeleka hospitalini zilifanyika lakini alifariki njiani kutokana na kuvuja damu nyingi.

Kamanda Nyigesa aliwataka raia kutii amri na kufuata sheria wanapoingia kwenye kambi za jeshi.