Asasi za kiraia Tanzania zapinga mabadiliko ya sheria

Monday June 24 2019

Mratibu wa Kituo cha Utetezi wa Mtandao wa Haki

Mratibu wa Kituo cha Utetezi wa Mtandao wa Haki za Binadamu nchini (THRDC), Onesmo Olengurumwa akisoma tamko la asasi za kiraia nchini zilizokutana jijini Dar es Salaam leo, kujadili Muswada wa marekebisho ya sheria ya Asasi hizo. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Muungano wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali Tanzania (TANGO), Ngunga Tepani na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la EFG, Jane Magigita na kulia ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Asasi za Kiraia (NACONGO), Ismail Suleiman. Picha na Ericky Boniphace 

By Peter Elias, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Asasi za Kiraia nchini Tanzania (Azaki) zimesema muswada wa mabadiliko ya sheria mbalimbali uliowasilishwa bungeni utakwenda kuua Azaki nchini humo kutokana na baadhi ya vifungu kuminya uhuru wa asasi hizo.

Hayo yamebainishwa na wadau wa Azaki leo Jumatatu Juni 24, 2019 wakati wakijadili upungufu kwenye muswada huo na kupendekeza kwamba muswada huo usijadiliwe kwa hati ya dharura ili wadau washirikishwe na kuujadili.

Akifafanua upungufu wa muswada huo, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa amesema muswada huo unazitaka Azaki zote zilizosajiliwa kama kampuni kufanya kazi kama kampuni ndani ya miezi miwili vinginevyo vitafutwa.

Pia, amesema muswada huo unampa nguvu waziri kutangaza kwamba NGO fulani imefutwa kwa kutoa tangazo kwenye Gazeti la Serikali. Amesema kifungu hicho kinaondoa utaratibu wa Baraza la Azaki kusimamia asasi hizo.

"Tunapendekeza muswada huu usijadiliwe chini ya hati ya dharura kwa sababu hakuna jambo la dharura. Tunaomba urudi kwetu wadau ili tujadiliane na kuona namna ya kuuboresha kwa maslahi ya Taifa," amesema Olengurumwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Usawa kwa Wasichana (EFG), Jane Magigita amesema Azaki zina mchango mkubwa kwa maendeleo ya Taifa, hivyo ni vema mabadiliko yoyote yanayofanywa na serikali yawashirikishe.

Advertisement

Advertisement