Asilimia 98 ya mbegu za pamba yawafikia wakulima

Muktasari:

  • Zaidi ya Sh4 bilioni kutumika kununua na kusambaza mbegu za pamba kwa wakulima na tayari asilimia 98 ya tani 12,000 za mbegu zimewafikia wakulima katika halmashauri 53 za mikoa 17 inayolima zao hili.

Bariadi. Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) imefanikiwa kusambaza asilimia 98 ya tani 12, 000 za mbegu za pamba kwa wakulima katika halmashauri 53 ya mikoa 17 inayolima zao hilo tayari kwa msimu wa kilimo unaoanza Novemba 15 kila mwaka.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Novemba 9, 2018 Mkaguzi Mwandamizi wa Pamba kutoka TCB, Renatus Luneja amesema asilimia mbili iliyosalia inatarajiwa kuwafikia wakulima ndani ya siku tano zijazo.

Alisema Serikali kupitia TCB na kwa ushirikiano na wadau wengine wa sekta ya pamba imefanikiwa kuzalisha tani 4,000 kati ya 6,000 za mbegu bora isiyo na manyoya aina ya UKM08 inayohitajika msimu huu.

"Kutokana na upungufu wa tani 2, 000 kulingana na matarajio, baadhi ya wakulima katika baadhi ya mikoa isipokuwa Geita, Tabora na wilaya za Sengerema mkoani Mwanza na Meatu mkoani Simiyu watatumia mbegu yenye manyoya ya UKMO8," amesema Luneja

Ofisa Uhamasishaji na Maendeleo ya Pamba kutoka TCB, Irene Marenge amesema upatikanaji na usambazaji wa mbegu unatarajiwa kugharimu zaidi Sh4 bilioni.

Meneja wa mbegu wa Kiwanda cha Quton (T) Ltd kinachozalisha mbegu bora ya UKM08, Phinias Chikaura amesema uzalishaji wa mbegu kwa wakati kulingana na mahitaji unakwamishwa na tabia ya baadhi ya wakulima kuuza pamba kidogo kidogo na hivyo kuchelewesha uchambuaji na upatikanaji wa mbegu ghafi.