Askari Magereza adaiwa kunaswa na pembe za ndovu

Wednesday April 3 2019

 

By Nazael Mkiramweni,Mwananchi [email protected]

Dodoma. Askari wa gereza la Msalato jijini Dodoma, anashikiliwa na polisi akituhumiwa kukutwa na vipande sita vya pembe za ndovu vyenye thamani ya Sh103.5 milioni.

Kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto leo Jumatano Aprili 3, 2019 amesema mtuhumiwa huyo alikamatwa Aprili mosi, 2019 katika mtaa wa Kilimani jijini humo akiwa na vipande hivyo vya pembe za ndovu vyenye uzito wa kilo 13 sawa na tembo watatu.

“Tulimwekea mtego askari huyo na tukafanikiwa kumkamata akiwa ameficha kwenye mfuko vipande vya pembe za ndovu kwa ajili ya kumsubiri mteja,” amesema Muroto.

Katika tukio lingine, Muroto amesema wanamshikilia mtu mmoja kwa tuhuma za kujifanya ofisa usalama wa taifa na kudanganya watu ili kujipatia fedha.

Amesema mtuhumiwa alikamatwa Machi 26,2019 jijini Dodoma akiwa na nakala za vyeti 15 vya watu mbalimbali, barua tatu za maombi ya ajira za watu tofauti na nakala ya leseni moja.

“Kabla ya kukamatwa alijipatia Sh950,000 kutoka kwa watu wawili, mmoja alimpatia Sh550,000 na mwingine alitoa Sh400,000 lengo ni kuwapatia ajira. Watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika,” amesema.

Advertisement

Kamanda Muroto amesema Serikali ina taratibu na mifumo yake ya kuajiri si kutumia watu au vishoka, hivyo amewataka kujihadhari na matapeli wa aina yoyote.

Advertisement