Askari aliyeuawa aacha mke anayetarajia kujifungua

Askari wa Jeshi la Polisi akiweka bendera ya jeshi hilo kwenye moja ya majeneza yenye miili ya polisi wanane wakati wa kuaga miili hiyo katika Chuo cha Polisi Kurasini jijini Dar es Salaam jana. Polisi hao waliuawa na watu wasiofahamika eneo la Jaribu wilayani Kibiti, Pwani juzi. Picha na Said Khamis

Muktasari:

Hayo yamebainika katika hafla ya kuaga miili ya askari nane waliouawa katika shambulio lililotokea Alhamisi jioni, huku kukiwa na taarifa nyingine ya kushambuliwa kwa mapanga kwa mtoto wa mwenyekiti wa Kijiji cha Kitembo wilayani Kibiti ambako mauaji dhidi ya viongozi na askari yanazidi kuongezeka.

Dar es Salaam/Pwani. Ayoub Mwaikambo, askari aliyeuawa katika shambulio dhidi ya gari la Jeshi la Polisi wilayani Kibiti, ameacha mke ambaye anatarajiwa kujifungua mwezi mmoja ujao.

Hayo yamebainika katika hafla ya kuaga miili ya askari nane waliouawa katika shambulio lililotokea Alhamisi jioni, huku kukiwa na taarifa nyingine ya kushambuliwa kwa mapanga kwa mtoto wa mwenyekiti wa Kijiji cha Kitembo wilayani Kibiti ambako mauaji dhidi ya viongozi na askari yanazidi kuongezeka.

Mtoto huyo, Saidi Abdallah alijeruhiwa kwa mapanga baada ya kukataa kuwatajia watu waliovamia nyumba yao usiku wa kuamkia jana, sehemu aliyojificha baba yake ambaye ni mwenyekiti wa kijiji hicho.

Jana, wakati wa hafla ya kuaga miili ya askari hao iliyofanyika Kurasini Barracks, Francisco Mwaikambo, ambaye ni kaka wa askari huyo, alisema amempoteza mtu ambaye alikuwa akijadiliana naye mambo ya familia.

“Ah! Ayoub amekufa wakati nilikuwa nimepata mtu mwingine wa kujadiliana naye mambo ya familia baada ya kukua na kufahamu umuhimu wa familia,” alisema Francisco huku midomo ikimcheza mithili ya mtu anayejizuia kulia. “Amemuacha mtoto wake tumboni.”

Habari zaidi soma Gazeti la Mwananchi