Breaking News

Askofu Shoo asema Askofu Mshemba hakupenda madaraka

Wednesday April 15 2020

 

By Alodia Dominick, Mwananchi [email protected]

Bukoba. Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo amesema aliyekuwa mkuu wa Kanisa hilo na Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Magharibi, Dk Samson Mshemba hakuwa akipenda madaraka.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatano Aprili 15, 2020 katika ibada ya mazishi ya Dk Mshemba yaliyofanyika katika kanisa ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini Magharibi mkoani Kagera.

Mazishi hayo yalihudhuriwa na watu wachache kwa ajili ya kuchukua tahadhari ya maambukizi ya corona jambo ambali lilisisitizwa na mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini Masharibi, Askofu Abelnego Keshomshahara.

Katika ibada hiyo iliyoongozwa na Shoo, alibainisha kuwa Dk Mshemba alistaafu baada ya kuongoza kanisa hilo kwa miaka 16, aliongezewa miaka miwili lakini alikataa na kutaka kuongezewa mwaka mmoja.

“Alikuwa mtu asiyependa madaraka nakumbuka tuliwahi kuahirisha uchaguzi ili aendelee kuongoza lakini kwa hekima zake alisema hawezi kuendelea, hakupenda madaraka alimheshimu kila mtu,” amesema.

Shoo amesema Askofu Mshemba alitaka kila mtu ajaribu kufanya kitu anachokiamini bila kubagua makanisa, alipenda kujitoa na kushirikiana  na wenzake.

Advertisement

Amesema katika kipindi chote cha miaka 16 alifanikiwa kuunganisha makanisa mbalimbali na kusaidia kupatikana wachungaji wa KKKT ukanda wa Afrika Mashariki, kudumisha amani, kudumisha vitengo mbalimbali vya makanisa vinavyotoa huduma za elimu, afya na miradi ya watoto.

Dk Shoo aliwataka watumishi wa Mungu kuendeleza mazuri yaliyofanywa na Askofu huyo na kuendeleza ushirikiano na watu wote bila kujali dini, jinsia na kabila.

Askofu mstaafu wa Kanisa la Anglikana jimbo la Bukoba,  Janton Rugumila amesema Askofu Mshemba atakumbukwa kwa kuunganisha makanisa mbalimbali katika kufanya maendeleo mkoani Kagera bila kujali madhehebu.

Mkuu wa mkoa wa Kagera,  Brigedia Jenerali Marco Gaguti alishiriki mazishi hayo na kuwasilisha salamu za Serikali na kuahidi kutoa ushirikiano na familia ya marehemu.

Askofu Mshemba alizaliwa Juni 30, 1935 katika kijiji cha Ruhanda kata ya Kamachumu wilaya Muleba na ameacha mjane na watoto saba.

Advertisement