BancABC yarahisisha biashara Tanzania, China kwa kadi maalumu

Mkuu wa Huduma za Kidigitali wa Benki ya BanABC, Silas Matoi (kulia), na Mkuu wa Wateja Binafsi na wateja wafanyabiashara wa kati na wadogo, Bi. Joyce Malai, wakionyesha mfano wa kadi ya ATM ya fedha za kichina wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa kadi hiyo jijini Dar es Salaam jana.

 

Muktasari:

Wakati biashara baina ya China na Tanzania ikiimarika, BancABC imerahisisha miamala ya Watanzania wanaotembelea China kwa kuanzisha kadi maalumu


Dar es Salaam. Wakati biashara baina ya China na Tanzania ikiimarika, BancABC imerahisisha miamala ya Watanzania wanaotembelea China kwa kuanzisha kadi maalumu.

Benki hiyo, imezindua kadi ya malipo ya kabla ijulikanayo kama Yuan pre-paid Visa card ambayo inawawezesha malipo kwa sarafu za China.

Mkuu wa kitengo cha dijitali cha BancABC, Silas Matoi amesema China ni kati ya nchi kubwa inayofanya biashara na mataifa mengi duniani ikiwamo Tanzania ambayo ina zaidi ya wanafunzi 6,000 wanaosoma nchini humo hivi sasa.

“Kadi ya Yuan inawawezesha watumiaji kupata fedha za Chinaa kwa thamani ile ile ambayo imewekwa kwenye kadi hivyo kupunguza changamoto za kubadilisha fedha ambazo wafanyabiashara na wanafunzi wamekuwa wakikumbana nazo wakiwa China,” amesema Matoi.

Kadi hiyo pia ina huduma ya kupokea ujumbe mfupi wa maneno kumpa mmiliki taarifa za kila muamala anaofanya mtandaoni na haina makato ya mwezi.

 “Mzazi mwenye mtoto anayesoma China anatakiwa kuweka fedha kwenye akaunti ya mwanaye yenye fedha za China  na papo hapo salio litaonekana kwenye kadi inayomilikiwa na mtoto wake,” amesema Matoi.

Mkurugenzi wa kitengo cha wateja binafsi na wanafanya biashara wa benki hiyo, Joyce Malai amesema kuzinduliwa kwa kadi hiyo ni mwendelezo wa huduma bora na zenye kutoa suluhisho kwa wateja.

Kadi hiyo inayopatikana kwa saa 24 kwa siku saba za wiki, inaweza kutumika kwenye zaidi ya mashine milioni 2.7 za kutolea fedha (ATM) zinazopokea kadi za Visa duniani kote pamoja na maduka milioni 46. Nchini, kuna ATM 400 na maduka 1,000 yanayokubali kadi hizo.

Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki amesema uhusiano wa kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili umeendelea kuimarika na biashara kati yao inashamiri.

 “Hivi sasa bidhaa za madini, kilimo na uvuvi kutoka Tanzania zinauzwa China.  Ujazo wa biashara kati ya China na Tanzania umefikia  Dola 4.3 bilioni za Marekani kwa mwaka,” amesema Mbelwa alipoulizwa MCL Digital kuhusu Taifa hilo la pili kwa uchumi mkubwa duniani kwa sasa.

Mbelwa amesema katika kipindi cha miaka miwili iliyopita China imefanikiwa katika utekelezaji wa miradi mipya 196 yenye thamani ya Dola 1.25 bilioni iliyowekezwa kwenye sekta za viwanda, makazi, kilimo na uvuvi.