Bashe aweka rehani ubunge wake

Muktasari:

Miradi iliyoanzishwa ndiyo inayompa ‘jeuri’

Ikiwa ni kipindi cha kwanza kuingia bungeni, Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe amesema iwapo atashindwa kutatua kero ya maji katika jimbo hilo hawezi kusimama na kuwaomba wananchi wamchague tena kuwa mbunge katika uchaguzi wa mwaka 2020.

Bashe alitoa kauli hiyo jana wakati akihojiwa katika kipindi cha 360 kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha Clouds.

Alisema tayari Nzega Mjini yenye watu 72,355 kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kuna miradi mbalimbali ya maji imeanza kutekelezwa, huku tatizo hilo likiendelea kupungua tofauti na miaka iliyopita.

Bashe alitaja miradi hiyo kuwa ni mradi wa Ziwa Victoria ambao hadi kukamilika kufika Tabora mjini, utagharimu zaidi ya Sh600 bilioni ambao utawezesha kuwa na mtandao mpya wa maji wa kilomita 45 katika mji wa Nzega.

Alisema aliomba Sh460 milioni kwa Rais John Magufuli kwa ajili ya maji, kati ya hizo tayari amepatiwa Sh250 milioni.

Alibainisha kuwa fedha hizo zimetumika kufanya ukarabati wa chujio la maji na kufufua Bwawa la Uchami, hivyo kuwawezesha wananchi kupata maji kwa mgawo mara mbili kwa wiki.

Pia, mbunge huya alisema Rais alipeleka Nzega Sh260 milioni nje ya bajeti ya halmashauri, ambazo zimetumika kujenga tangi lililopo Shule ya Msingi Nyasa na kujenga vituo vya maji katika maeneo mbalimbali ya Nzega.

Alisema miradi mingine ni ya visima 13 vinavyotumia umeme jua katika maeneo ambayo mradi wa maji wa Ziwa Victoria hautafika.

“Tunaamini miradi yote hii hadi 2020 itakuwa imekamilika kwa kuwa mbali na hiyo, nilishaomba msaada Japan wa uchimbaji wa visima sita. Kama miradi hii yote haitakamilika sina haja ya kwenda kuwaomba kura wananchi wa Nzega,” alisema Bashe.