Bashiru Ally aeleza faida za mijadala ya kisiasa, amjibu Lowassa

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally (kushoto) na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji wakifurahia jambo wakati wa kongamano la kigoda cha Mwalimu Nyerere linalofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam leo. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema mijadala ya kisiasa ina faida tatu ambazo ni kubadilisha mazoea mabaya kwa jamii, kudumisha mazoea mazuri na kubuni mazoea mapya


Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa CCM, Dk Basiru Ally amesema mijadala ya kisiasa ina faida tatu, ambazo ni kubadilisha mazoea mabaya kwa jamii, kudumisha mazoea mazuri na kubuni mazoea mapya.

Dk Bashiru ameyasema  hayo leo wakati  akichangia mada katika mdahalo wa miaka 19 ya kumbukizi ya kifo cha Mwalimu Julius Nyerere.

Amesema mijadala ni kama damu na mwili na kwamba mwenye jukumu la kufanya kazi ya kuendesha mijadala hiyo kwa nchi masikini kama Tanzania ni vyuo vikuu vya umma.

“Mimi kama Katibu Mkuu wa CCM nitapigia debe bajeti kwenye vyuo vikuu vya umma ili viweze kuzalisha wasomi watakaotukomboa kifikra na kimaendeleo,” amesema Bashiru.

Katibu Mkuu huyo wa CCM amesema yupo tayari kujadiliana na wanasiasa wenzake lakini si kwa kugombania mgawanyo wa madaraka ndani ya vyama ambayo baada ya kuyapata yanatumika kufanya matumizi ya anasa.

“Mijadala itatufanya tujisahihishe tumekosea sana, tumepotea sana na mbaya zaidi tumeanza kuogopa kusema ukweli, ” amesema.

Kuhusu kuwapo kwa hofu miongoni mwa wananchi katika chaguzi ndogo, hoja ambayo ilizungumzwa na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa katika mdahalo huo, Dk Bashiru amesema ni kweli lakini hofu hiyo ipo kwa wezi wa mali ya umma, wakwepa kodi,  matapeli wa kisiasa, walioingia  mikataba ya kuiba mali za umma, madalali na  makuwadi wa soko huria.

Amesema hofu halisi ya Watanzania ni maji safi, elimu bora, haki mahakamani na siyo hofu nyingine za kupandikiza.

Kuhusu kutumika askari wakati wa uchaguzi kama ambavyo ilielezwa na Lowassa,  amesema wanachama wa CCM na Chadema  ni kama maadui na wakati mwingine wanashikiana silaha hivyo si rahisi polisi kukaa kimya.

“Kwangu wanachama hao wapo na kwako pia wapo, wamekuwa maadui, wanashikiana silaha. Haiwezekani polisi wasichukue hatua wakae ndani, watakuwa hawajatimiza wajibu wao, ”amesema Bashiru.

Soma zaidi: