Bei nyumba za NSSF zashtua Kamati ya Bunge

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara, bei za nyumba za Dege ni kati ya Dola za Marekani 110,000 (Sh220 milioni) hadi Dola 250,000 (Sh500 milioni) kulingana na aina ya nyumba.

 Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) wameshtushwa na bei ya kuuza nyumba za mradi wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) zilizoko eneo la Dege Kigamboni jijini Dar es Salaam wakisema haziendani ya hadhi na hali ya wananchi walio wengi.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara, bei za nyumba za Dege ni kati ya Dola za Marekani 110,000 (Sh220 milioni) hadi Dola 250,000 (Sh500 milioni) kulingana na aina ya nyumba.

Wakizungumza jana baada ya kutembelea miradi ya NSSF jijini Dar es Salaam, wabunge hao walitilia shaka uuzwaji wa nyumba hizo huku shirika hilo likikiri kutozitangaza mapema kwa wateja.

Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka alisema nyumba za mradi wa Dege hazina hadhi ya kuuzwa bei hiyo.

“Ukiangalia nyumba zenyewe zina ‘poor quality’ (kiwango cha chini), hata ukiangalia ‘design’ yake sio nzuri. Vyumba ni vidogo, hivi kweli mtu atashawishika kutoa Sh200 milioni kununua nyumba hiyo?” alihoji Kaboyoka.

Hoja hiyo, iliungwa mkono na Mbunge wa Magomeni Zanzibar, Jamal Kassim akisema hazikujengwa kwa kuwalenga watu wa kipato cha chini.

“Hizi nyumba hazikujengwa kwa ajili ya watu wa kipato cha chini, bali wenye kipato cha juu hasa wageni. Hata hivyo, kwa kuwa wameshawekeza fedha lazima mradi ukamilike na nyumba ziuzwe,” alisema.

Mbunge wa Viti Maalumu Dodoma, Felister Bura alihoji upatikanaji wa wateja ikiwa watumishi wa umma wanaotegemewa wengi wao wanahamia Dodoma ambako ndiko makao makuu ya nchi.

Akijibu hoja na maswali ya wabunge, Profesa Kahyarara alisema nyumba hizo za Dege zitauzwa kati ya Dola 110,000 hadi Dola 125,000 kwa moja na Dola 195,000 hadi Dola 250,000 kwa nyumba aina ya villa.

Alisema mteja atatakiwa kulipa kwa muda wa miaka sita.

Mbali na mradi wa Dege, NSSF pia iliwaonyesha wajumbe hao wa PAC mradi wa Dungu, ambao Profesa Kahyarara alisema una nyumba 439 na umegharimu jumla ya Sh89.5 bilioni.

“Mradi wa nyumba hizo utakamilika Juni mwaka huu na mpaka sasa tumeshatumia Sh50 bilioni,” alisema Profesa Kahyarara.

Kuhusu mradi wa Toangoma wenye nyumba 161, mkurugenzi huyo alisema umetumia gharama ya Sh61 bilioni.

Hata hivyo, Profesa Kahyarara alikiri kutozitangaza nyumba hizo mapema jambo lililozua maswali kwa wabunge kuhusu uhakika wa kuziuza.

Mbali na bei hizo, pia imeelezwa kuwa mvutano wa hisa kati ya NSSF na kampuni ya Azimio ni chanzo mojawapo cha kucheleweshwa kwa mradi wa nyumba zaidi ya 7,000.

Profesa Kahyayara aliiambia kamati hiyo kuwa mradi huo umeshatekelezwa katika awamu mbili na nyumba 3,750 zimeshakamilika kati ya 7,160 za mradi mzima.

Kwa mujibu wa mkataba huo, kampuni ya Azimio iliyotoa ardhi ya hekta 300 inamiliki hisa asilimia 55 huku NSSF iliyowekeza zaidi ya Dola 500 ikimiliki hisa asilimia 45.

Alisema mradi huo ulitarajiwa kukamilika mwisho wa mwaka huu lakini haitawezekana kutokana na dosari za mkataba. Baadhi ya wajumbe wa PAC walihoji sababu ya mkurugenzi wa kampuni ya Azimio kutoonekana kila anapotafutwa.

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Kilimanjaro, Shaly Raymond alisema kuchelewa kwa mradi huo kutapandisha gharama kutoka Dola 544 milioni hadi 700 na kuhoji nani atakayelipa, huku pia akihoji sababu za mwekezaji wa Azimio kutokuwapo katika ziara hiyo.

“Angalia hiyo meza kuu, mwekezaji hayupo, wewe mkurugenzi umekuja peke yako, wenzako wako wapi?” alihoji Shaly.

Mbunge Bura alisema kama Azimio hawataki kuonyesha ushirikiano, atafutwe mwekezaji mwingine. “Tulipozungumza na mwekezaji huyu alikubali kupunguza hisa zake kwa sababu amewekeza kidogo. Kama anasumbua, NSSF waangalie namna ya kupata mwekezaji mwingine.”

Akijibu hoja za wabunge, Profesa Kahyarara alikiri kucheleweshwa kwa mradi huku akisema bado wanajadiliana na kampuni ya Azimio.

Alimtetea mwekezaji huyo akisema amekuwa na safari nyingi nje ya nchi na kwamba atakuwepo kwenye kikao cha Januari 26 na mambo yote yatajadiliwa na kutolewa uamuzi.