Benki ya NBC yatoa mbinu za biashara kwa wanawake wa Kiislam

Tuesday January 28 2020

 

By Bakari Kiango, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Benki ya Biashara ya NBC imezindua mpango maalumu wenye lengo la kuwajengea uwezo wajasiriamali.

Hayo yalielezwa jana katika mkutano wa kwanza wa wanawake wa Kiislam kuhusu ujasiriamali na Tanzania ya viwanda na mkuu wa kitengo cha wateja maalumu rejareja wa NBC, Ashura Waziri.

Ashura alisema kupitia mtandao wa Klabu ya Biashara ya NBC, wajasiriamali wanawake hususan wanaoanzisha biashara na wenye shauku ya kuanzisha viwanda, wanayo fursa ya kujiunga na klabu hiyo ili kunufaika za mafunzo yanayotolewa bila malipo kuhusu mbinu za ujasiriamali kwa vitendo.

Semina hiyo iliandaliwa kwa uratibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) na kudhaminiwa na NBC.

Akihutubia zaidi ya wanawake 3,000, Ashura alisema wamewajengea uwezo wajasiriamali wengi kwa kutoa mafunzo hayo yanayofanywa kwa ushirikiano na taasisi za umma na binafsi.

“Tunafanya programu zote za kuwajengea uwezo wafanyabiashara kupitia Klabu ya Biashara NBC tunahamasisha wenye mahitaji ya kupata mbinu za biashara kuwasiliana na matawi yetu yote nchini,” alisema Ashura.

Advertisement

Akifungua semina hiyo kwa niaba ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angela Kairuki alisema Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wanawake kuwekeza katika miradi.

Katika hafla hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Zungu aliwataka wanawake kuweka vizuri mapato yao na kuwekeza badala ya kutumia fedha hizo kwa matumizi yasiyo na umuhimu.

NBC ilianzisha dirisha maalumu kutoa huduma za benki kwa kufuata misingi na kanuni za Kiislam, ikitoa huduma na bidhaa mbalimbali zikiwamo akaunti za muda maalumu.

 

 

Advertisement