Benki zashindana kushusha riba, kuvutia wakopaji

Muktasari:

Hata wafanyakazi wenye kipato cha chini, sasa wanapewa fursa ya kukopa fedha nyingi baada ya benki kadhaa kuanza kupunguza riba

Dar es Salaam. Wafanyakazi wamekuwa shabaha ya kwanza ya benki za biashara zinazoshindana kuongeza wateja kwa riba nafuu.

Hata wafanyakazi wenye kipato cha chini, sasa wanapewa fursa ya kukopa fedha nyingi baada ya benki kadhaa kuanza kupunguza riba.

Katika kufanikisha hilo, kwa siku za karibuni, benki zimeshuhudiwa zikipunguza riba, kuongeza muda wa marejesho na kupandisha kiwango cha mkopo huku zikiwapa nafasi hata wafanyakazi wenye kipato cha chini.

Jana, Benki ya CRDB ilitangaza kuongeza kiasi cha mkopo kwa wafanyakazi huku ikipunguza riba kutoka asilimia 22 hadi 16.

Neema hiyo inampa mfanyakazi fursa ya kukopa mpaka Sh100 milioni tofauti na zamani kikomo kilipokuwa Sh50 milioni na kuruhusiwa kurejesha mpaka miaka saba kutoka minne ya awali.

Mkurugenzi mtendaji wa benki hiyo, Dk Charles Kimei alisema jana kuwa, wamepunguza riba ili kutoa unafuu wa mikopo kwa wateja wao jambo litakalosaidia kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja na uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Taasisi nyingine zilizofanya hivyo ni Benki ya Afrika (BoA) inayotoza asilimia 11 kwa watumishi wa Serikali na mkopo kuanzia Sh1 milioni mpaka Sh30 milioni na NMB inayotoza riba ya asilimia 17.

Mabadiliko hayo yanafanywa baada ya miaka miwili ya kuyumba kwa sekta ya fedha nchini kutokana na kuelemewa na mikopo isiyolipika na kupungua kwa mikopo ya sekta binafsi.

Wadau wanasemaje?

Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Ernest Kitindi alisema mchango wa sekta binafsi ni muhimu kwenye uchumi wa Taifa na kwamba baada ya wafanyakazi, anaamini wafanyabiashara nao watapunguziwa.

“Sekta ya fedha ina ushindani mkubwa sana sasa hivi. Wafanyakazi wanaonekana kuwa na kipato cha uhakika kidogo kwa sasa tofauti na wafanyabiashara. Nadhani benki zinaangalia mwenendo wa biashara kabla ya kuanza kuwakopesha wajasiriamali pia,” alisema Profesa Kitindi.

Kuhusu mwenendo wa baadhi ya biashara kufungwa huku nyingine zikipunguza wafanyakazi, alisema: “Kila mkopo huwa na bima. Wafanyakabiashara hulipia zaidi kuliko wafanyakazi.”

Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Tumaini Nyamhokya amezipongeza benki kwa hatua hiyo akisema itasaidia kuboresha kipato cha wafanyakazi watakaokuwa makini.

“Benki zinafanya biashara kubwa na wafanyakazi. Baadhi walikuwa wamefika ukomo wa kukopesheka na wachache walikuwa hawakopesheki kabisa. Kwa kupunguza riba na kuongeza muda wa marejesho, wengi watanufaika zaidi,” alisema Nyamhokya.

Pamoja na fursa hiyo, rais huyo aliwataka wafanyakazi watakaokopa kuwekeza ili kuongeza kipato chao kwa ajili ya kukidhi mahitaji yao muhimu.

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilishusha riba ya mikopo inayotoa kwa benki za biashara kwanza. Machi mwaka huu ilitangaza kupunguza riba hiyo kutoka asilimia 16 hadi 12. Mwaka mmoja baadaye ikashusha tena mpaka asilimia tisa.

Licha ya riba ya mikopo, BoT pia ilishusha uwiano wa kiasi cha fedha ambacho benki za biashara na taasisi za fedha zinatakiwa kutunza kwake (statutory minimum reserve ratio) kutoka asilimia 10 mpaka nane ili kuziwezesha kukopesha zaidi.

Vilevile, BoT imekuwa ikipunguza riba kwenye hatifungani za Serikali ambayo sasa imefikia asilimia nne kutoka zaidi ya asilimia 10 iliyokuwapo Mei mwaka jana ili kuzishawishi benki kujielekeza zaidi sekta binafsi.

Hayo yanafanyika baada ya sekta ya fedha kusuasua miaka miwili iliyopita huku benki nyingi zikielemewa na mikopo isiliyolipika iliyoathiri mitaji hata baadhi kushindwa kujiendesha, hivyo kufutiwa leseni za biashara kutokana na kutokidhi matakwa yanayokubalika kisheria.