Bomoabomoa njia ya reli yasababisha kilio Mwanza

Muktasari:

  • Hata hivyo, tofauti na vilio vya baadhi ya wananchi wengine wanaokumbwa na adha kama hiyo, baadhi ya wafanyabiashara hao walikiri kuvamia eneo hilo tangu mwaka 1994 baada ya reli hiyo kuacha kufanya kazi.

 Wakati kampuni hodhi ya rasilimali za reli nchini (Rahco) ikianza utekelezaji wa kubomoa nyumba zote zilizojengwa ndani ya njia ya reli, zaidi ya wafanyabiashara 200 wa samaki na dagaa jijini Mwanza hawana pa kwenda baada ya kubomolewa vibanda vyao.

Hata hivyo, tofauti na vilio vya baadhi ya wananchi wengine wanaokumbwa na adha kama hiyo, baadhi ya wafanyabiashara hao walikiri kuvamia eneo hilo tangu mwaka 1994 baada ya reli hiyo kuacha kufanya kazi.

Kutokana na hatua hiyo, mfanyabiashara wa samaki eneo la Stesheni na Bandarini, Maige Wambura aliiomba halmashauri kuwatafutia eneo lingine litakalofaa kwa biashara ili wajipatie kipato.

“Ni kweli hatukuwa na eneo maalumu ndio maana tulikuwa hapa tukifanya biashara zetu, lakini leo (jana) tumebomolewa na hatujaelekezwa tunaenda wapi,” alisema Wambura.

Wambura alisema watu wapatao 17 walikuwa na vibanda kwenye njia hiyo na kulikuwa na wakaanga samaki takriban 67, mamalishe 83 na wauzaji wa matunda zaidi ya 40.

Ofisa Mfawidhi wa Rahco, Daimon Mwakaliki alisema ubomoaji huo ni utekelezaji wa mpango wa Serikali kupisha ujenzi wa reli ya kisasa ya (Standard Gauge).

Bila kutaja idadi ya nyumba za watu, taasisi za Serikali na zisizo za kiserikali, kidini, shule na viwanja vya michezo, zitakazoathirika, Mwakaliki alisema utekelezaji huo umeanza ikiwa ni siku tatu tangu Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuagiza kuanza ubomoaji huo.

Alisema watakaobomolewa ni wale waliojenga ndani ya mita 15 kutoka stesheni ya reli hadi bandarini na kutoka njia kuu ya reli na kuendelea, itakuwa mita 30.

“Zoezi hili si la kushtukizwa kwani tulitoa notisi kwa watu wote waliovamia miezi sita iliyopita, baadhi yao walibomoa wenyewe lakini baadhi walikaidi ingawa pia juzi tulipita kwenye maeneo yote yatakayobomolewa kuwatangazia kuanza kuwabomolea,” alisema Mwakaliki.

Bomoabomoa hiyo imeukumba ukuta wa Uwanja wa Nyamagana, ukuta wa Mamalaka ya Bandari, kiwanda cha samaki cha Vicky na taasisi nyingine yakiwamo makanisa na nyumba za kawaida.

Kazi hiyo ya ubomoaji ilidumu kwa saa saba ikifanywa chini ya ulinzi mkali wa polisi waliokuwa waliokuwa na silaha.