Bunge kutofanya maamuzi Ijumaa

Muktasari:

Hatua hiyo inatokana na siku hiyo wabunge wengi kwenda kuswali na Bunge kubaki na wachache

Dodoma. Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema kuanzia sasa chombo hicho cha kutunga sheria hakitafanya maamuzi yoyoote kuhusu mambo mbalimbali siku za Ijumaa.

Uamuzi huo umetokana na mwongozo ulioombwa leo na Mbunge wa Baraza la Wawakilishi (CCM), Jaku Hashim Ayub.

Mbunge huyo aliomba siku za Ijumaa saa 6.00 mchana shughuli za Bunge ziwe zinaahirishwa ili kuwapa nafasi wabunge wa dini ya Kislamu kwenda msikitini.

Alisema hiyo ni mara ya tatu kwa yeye kulizungumzia jambo hilo bungeni na kwamba historia itamkumbuka.

“Tufanyiwe haki hili Bunge linaitwa la Jamhuri ya Muungano, sio Bunge la Tanzania, mheshimiwa Spika busara zako na jicho lako la rehema naomba uangalie kanuni ya 153 ili suala hili ulipatie ufumbuzi,” alisema.

Akijibu mwongozo huo, Spika Ndugai alisema hilo ni jambo kubwa na kwamba Bunge haliwezi pekee yake kujiamulia kwa kubadili utaratibu wa siku za Ijumaa.

“Bunge sisi ni viongozi maana yake ni kwamba tutaifanya mahakama nayo kutokufanya kazi saa fulani Ijumaa na Serikali nayo ianze kufikiri hivyo,” alisema.

Alisema jambo hilo linahitaji uamuzi mpana wa pamoja na kwamba kuamua pekee yao (Bunge) kuna weza kukawapa matatizo.

“Ni jambo muhimu tuendelee kulifanyia kazi tutafika mahali tutakubaliana. Lakini kwa hatua ndogo ndogo ambazo tutachukua sisi kama Bunge hapa siku hiyo ya Ijumaa kwa saa zile za Ibada tutaepusha kuwa na kura ya uamuzi,” alisema.

Hata hivyo, Ndugai alisema wakati ambapo kuna shughuli za michango bungeni, kikao kitaendelea isipokuwa wakati wa kutoa uamuzi.