CRDB yatoa Sh100 milioni kuboresha JKCI

Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Profesa Mohammed Janabi.

Muktasari:

Kwa sasa wagonjwa wengi wanalazimika kusubiri kutokana na ufinyu wa eneo.

 

Dar es Salaam. Uboreshaji wa majengo mapya ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) utaongeza idadi ya wagonjwa wengi watakaotibiwa kwa wakati, tofauti na ilivyo sasa.

 

Kwa sasa wagonjwa wengi wanalazimika kusubiri kutokana na ufinyu wa eneo.

 

Hayo yamesemwa leo Juni 14 na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Profesa Mohammed Janabi mara baada ya kupokea hundi ya Sh100 milioni iliyotolewa na Benki ya CRDB kama mchango wa ujenzi huo unaohitaji zaidi ya Sh900 milioni.

 

Profesa Janabi amesema kwa sasa kumekuwa na ufinyu wa eneo kutokana na kitengo hicho kupokea wagonjwa wengi wanaowahudumia hasa watoto wadogo.

 

“Vyumba vya uangalizi maalum (ICU) kuna ufinyu na hata wodi za watoto hazitoshi, hapa kwetu asilimia 60 ya tunaowafungua vifua kwa ajili ya upasuaji wa moyo ni watoto na watu wazima ni asilimia 40. Hivyo tuna uhitaji wa wodi za watoto na ICU,” amesema.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dk Charles Kimei amesema kwa kutambua umuhimu wa afya kwa Watanzania benki hiyo inatarajia kutoa kadi maalumu za benki za matibabu ambazo wagonjwa watazitumia kutibiwa pasipo kutembea na fedha taslimu.