China kunoa kwa vitendo wahitimu UDSM

Monday June 24 2019

By Kelvin Matandiko, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Serikali ya Jamhuri ya watu wa China imezindua darasa la mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi na wahitimu katika fani za uhandisi, teknolojia na ubunifu nchini Tanzania liitwalo Lu Ban Workshop, ikiwa ni sehemu ya kuenzi jina la Mchina Lu Ban, aliyeeneza teknolojia ya viwanda China.

Jukwaa hilo litafanya kazi ya kunoa wahitimu hao ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Taasisi ya Mafunzo ya Utamaduni wa Kichina, Confucius institute (CI) na Umoja wa Kampuni zaidi ya 600 za Kichina hapa Tanzania.

Akizungumza leo Jumatatu asubuhi Juni 24, 2019 Jijini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa darasa hilo, Makamu wa Rais wa Taasisi ya Mafunzo ya Uhandisi nchini China ya Chongqing, Profesa Wu Zaisheng amesema darasa hilo litakuwa na mageuzi katika ukuzaji wa sekta ya uhandisi na teknolojia.

“Itakuwa ni fursa kwa wanafunzi watakaofanya vizuri kwenda kuendelezwa ujuzi wao katika vyuo vya China, hatuangalii gharama za ushiriki wa mwanafunzi ila tutachukua mwenye uhitaji,” amesema Profesa Wu.

Mkurugenzi Mtanzania wa CI, Profesa Aldin Mutembei amesema Tanzania itakuwa nchi ya kumi kupata heshima ya Serikali ya China kuanzisha jukwaa hilo ili kunoa ujuzi kwa vitendo katika kampuni zaidi ya 600 za Kichina hapa nchini na kuwaendeleza kimasomo.

“Utaratibu na sifa za kuwapata wahitimu, muda wa kupata mafunzo pamoja na hatua nyingine zitaanza kujadiliwa kuanzia leo , tutaangalia tufanye mafunzo kwa miezi miwili au mitatu,”amesema Profesa Mutembei.

Advertisement

Akizungumza kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Mwanasheria Mkuu, Dk Saudin Mwakaje  amesema kati ya wanafunzi 20 hadi 50 wataanza kunufaika na jukwaa hilo litakalotoa mafunzo ya vitendo kwa kozi mbalimbali za uhandisi ikiwa ni hatua ya kwanza ya makubaliano ya miaka mitano.

Advertisement