China kutoa mabilioni ya fedha Afrika

Muktasari:

Mabilioni hayo yamo kwenye mpango wa miaka mitatu wa China katika ushirikiano wake na Afrika

Dar es Salaam. Rais wa China, Xi Jinping amesema nchi hiyo itatoa jumla ya dola bilioni 60 za Marekani sawa na Sh137 trilioni kwenye mpango wake wa miaka mitatu ya ushirikiano na Afrika katika shughuli za maendeleo. 

Rais Jinping amesema hayo leo Jumatatu, Septemba 03, 2018 wakati akifungua mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) unaofanyika jijini Beijing nchini China.

Taarifa kwa umma iliyotolewa na ofisi ya Waziri Mkuu imesema Rais Jinping ameahidi kuwa nchi yake itatoa ushirikiano ili kuhakikisha amani ya kudumu inapatikana Afrika, hatua ambayo ni muhimu kwa ustawi wa nchi za Afrika.

Maeneo mengine ambayo Rais huyo ameahidi kuwa China italisaidia bara la Afrika ni pamoja na ujenzi wa miundombinu, ushirikiano katika sekta ya biashara na huduma za afya.

Rais Jinping amesema China itatoa nafasi za mafunzo ya kilimo bora na mafunzo ya ufundi kwa wataalam kutoka nchi za Afrika ili kuchangia katika maendeleo ya uchumi.

Amesema kwa sasa anaamini China na nchi za bara la Afrika wako karibu zaidi na wanashirikiana vizuri katika shughuli za kimaendeleo ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Katika mkutano huo ulioanza kwa sherehe ya ukaribisho na baadaye viongozi kutoka nchi mbalimbali barani Afrika na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres walipata fursa ya kupiga picha ya pamoja na mwenyeji wao Rais wa China.

Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa ambaye anamuwakilisha Rais John Magufuli katika mkutano huo alisalimiana na Rais Jinping baada ya ufunguzi.

Mkutano huo utaendelea kesho ambapo viongozi wengi kutoka Bara la Afrika watapata nafasi ya kuzungumza.