DC Kinondoni ataka uchunguzi tuhuma mwalimu kunajisi wanafunzi

Muktasari:

Jeshi la Polisi linaendelea na upelelezi 

Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Salum Hapi ameliagiza Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tuhuma za mwalimu wa kiume katika Shule ya St Florence ya jijini Dar es Salaam kudaiwa kuwanajisi wanafunzi.

Ameagiza kutafutwa na kukamatwa kwa mwalimu huyo   anayetuhumiwa kufanya vitendo hivyo ambaye tangu Machi 16, 2018 haonekani shuleni hapo.

Tangu jana jioni kumekuwa na taarifa za mwalimu mmoja wa shule hiyo kuwanajisi watoto wanne wa darasa la saba, jambo lililozua taharuki.

Mkuu huyo wa wilaya alipowasili shuleni hapo alipokewa na mwalimu mkuu,  Wilson Mwabuka huku baadhi ya walimu wakitimua mbio na kujifungia wakihofia kupigwa picha.

Akizungumza baada ya kutembelea shule hiyo, Hapi aliwataka wazazi na jamii kuwa watulivu wakati polisi wakiendelea na uchunguzi.

"Walimu, wanafunzi na watumishi wa shule ni binadamu na kila binadamu ana hulka zake ndio maana tunazo sheria kwa kuwa makosa hayawezi kutotokea. Makosa ya walimu yasichanganywe na makosa ya taasisi, tuiache taasisi iendelee kutoa elimu," amesema.

Awali,  Mwabuka alisema tayari Jeshi la Polisi linaendelea na upelelezi hivyo hataweza kuzungumzia jambo hilo.

Amesema tangu Machi16, 2018 mwalimu huyo hajaonekana shuleni.

"Kwa hiyo kwa sababu mimi siyo mwanasheria siwezi kuzungumza, nawaomba wazazi na jamii kusubiri polisi kwa sababu wanaendelea kufanya uchunguzi na wameshatuhoji," amesema.