DC aahidi kupambana na waume wanaopiga wake zao

Muktasari:

  • Akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni ya ujenzi wa madarasa ya Shule ya Sekondari Tagamenda wilayani hapa, Kasesela alisema amechukua uamuzi huo kutokana na baadhi ya familia kuchukulia vitendo hivyo kuwa ni vya kawaida.

Iringa. Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela amepiga marufuku vitendo vya wanaume walio kwenye ndoa kupiga wake zao, akisema atakayebainika hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni ya ujenzi wa madarasa ya Shule ya Sekondari Tagamenda wilayani hapa, Kasesela alisema amechukua uamuzi huo kutokana na baadhi ya familia kuchukulia vitendo hivyo kuwa ni vya kawaida.

Alisema hadi sasa ameshawakamata na kuwachukulia hatua za kisheria wanaume watatu na kuwataka wanawake wanaopatwa na masaibu hayo kutoa taarifa kwake ili achukue hatua badala ya kuona kuwa vitendo hivyo ni sehemu ya maisha yao.

Hata hivyo, hakutaja majina ya wanaume hao aliowashughulikia kwa kupiga wake zao.

“Ninatangaza vita na wanaume wote wanaopiga wake zao. Mimi sitaki kubeba dhambi zenu, yeyote anayemtwanga mke wake nitapambana naye,” alisema Kasesela.

Alisema hakuna mafanikio yanayoweza kupatikana katika familia endapo mama na baba wanaingia katika ugomvi na hata kuumizana.

Hatua ya Kasesela kuwataka wanawake kutoa taarifa ilipokewa kwa furaha na wanawake waliohudhuria mkutano huo ambao walisema itasaidia kurejesha amani katika nyumba zao.

Mmoja wa kinamama hao, Rehema Gabriel alisema vitendo vya unyanyasaji wa wanawake vimekuwa vikiongezeka licha ya kuwapo kwa dawati la jinsia katika kituo cha Polisi.

Alisema kitendo cha mkuu huyo wa wilaya kuingilia kati kitasaidia kukomesha tabia ya wanaume wanyanyasaji.

Jeshi la Polisi limeweka dawati maalumu katika vituo vyake kwa ajili ya kushughulikia masuala hayo ya unyanyasaji katika ndoa.

Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa wilaya amewataka wananchi kujenga utamaduni wa kuwafundisha watoto wao namna ya kujitunza ili kupunguza maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).

Alisema licha ya kuwaelimisha kwa kipindi cha mwaka uliopita, bado hali ya maambikizi wilayani kwake na mkoani kwa ujumla yako juu na kutaka ufike wakati wazazi wawafundishe watoto kuhusu masuala ya uhusiano bila woga ili kukinusuru kizazi kijacho.

“Tuondoe woga tuwafundishe watoto wetu kuhusu mabadiliko ya miili yao na uhusiano kwa ujumla waelekezwe namna ya kujitunza na wale wanaoshindwa watumie kondomu,” alisema Kasesela.