DED Kongwa afariki ajalini, gari lake labinywa na lori la mafuta

Muktasari:

Mganga mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Caroline Damian alithibitisha kupokea mwili wa Ngusa ambao umehifadhiwa katika chumba cha maiti cha hospitali hiyo.

 Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, Izengo Ngusa amefariki dunia jana katika ajali ya gari iliyohusisha lori la mafuta lililoliangukia gari dogo binafsi eneo la Mbande, Makalavati wilaya humo.

Mganga mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Caroline Damian alithibitisha kupokea mwili wa Ngusa ambao umehifadhiwa katika chumba cha maiti cha hospitali hiyo.

“Ameumia zaidi kichwani, mkono na mguu wa kushoto,” alisema Damian.

Akizungumzia kifo cha Ngusa, mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Chamwino, Athuman Masasi alisema kimewasikitisha kwa kuwa wamepoteza mtu mwadilifu, mcheshi na mtendaji.

Alisema enzi za uhai wake Ngusa alikuwa mhandisi kitaaluma na kwa hiyo walikuwa wakishirikiana naye kwa mambo mengi.

“Tulishirikiana kwa karibu kiutendaji kwa sababu alikuwa ni mhandisi, alinishauri na tulishauriana kwa mambo mengi,” alisema.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kongwa, White Zuber alisema Ngusa alikuwa mtu makini na mwenye mchango mkubwa katika maendeleo ya wilaya hiyo.

“Tumepoteza mtu muhimu katika maendeleo, aliwezesha halmashauri kupata hati safi. Tutamkumbuka kwa mengi,” alisema.

Mkuu wa wilaya hiyo, Deogratius Ndegembi alisema ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamkia jana na taarifa ziliwafikia asubuhi.

Alisema kutokana na mazingira ya ajali, kazi ya uokoaji ilichukua muda mrefu mpaka jana jioni ndipo mwili ukanasuliwa kutoka katika eneo la tukio kwa kushirikisha vikosi vya Jeshi la Zimamoto na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).