VIDEO: DOROTH Katibu mkuu ACT anayetamani ubunge 2020

Doroth Semu

Muktasari:

ACT Wazalendo, ambayo kirefu chake ni Alliance for Change and Transparency, ni chama cha kisiasa kilichoanzishwa na kupata usajili wa kudumu 2014 na kinaunganisha nguvu kupigania mabadiliko na uwazi, kikiwa chini ya mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe..


Ni mwanamke mrembo, mwenye ngozi ya rangi ya maji ya kunde na nywele zilizosokotwa kwa mtindo wa rasta, pia akiwa na sifa ya ziada; kiongozi wa juu na mtendaji mkuu wa chama cha siasa.

Ni Doroth Semu, mama wa watoto watatu, wawili kati yao wa kiume. Kwa sasa ndiye katibu mkuu wa chama cha siasa cha ACT- Wazalendo.

Ukikutana naye huwezi kufikiri anaijua vizuri siasa, lakini ukipata nafasi ya kuzungumza naye utamkubali kutokana na uwezo wake wa kujenga hoja na kujibu maswali ya masuala mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.

Doroth aliteuliwa mwaka mmoja uliopita kushika wadhifa huo wa juu baada ya aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho, Samson Mwigamba kujiuzulu na baadaye kutimkia CCM.

Katika mahojiano na Mwananchi hivi karibuni, mtendaji huyo mkuu wa ACT-Wazalendo anasema kuingia kwake katika siasa si jambo la bahati mbaya.

Si hivyo tu; kwa sasa anafanya maandalizi ya kujitosa kuwania ubunge jijini Dar es Salaam.

Doroth anasema kuingia kwake katika siasa kunahusiana na historia ya maisha yake tangu akiwa shuleni. Hapo ndipo anapovuta kumbukumbu za historia yake.

“Shule ya msingi nilisoma Arusha School. Kama unavyojua shule za aina hii zina kila kitu. Chakula kizuri. Kuna mpaka swimming pool (bwawa la kuogelea),” anasema Doroth katika mahojiano na Mwananchi yaliyofanyika ofisi za makao makuu ya Mwananchi Communications Limited.

“Hapa sikuwahi kujua kama kuna watoto wengine wanapata shida. Namshukuru mama yangu. Wakati shule ilipokuwa ikifungwa alikuwa akitupeleka kusoma shule za kawaida, na mimi nikasoma Shule ya Msingi Sanawari huko ndipo nilipogundua kuwa kuna maisha mengine.

“Tangu hapo, niligundua kuwa hawa Watanzania wanapaswa kupata watu wa kuwawakilisha ili kuboresha maisha yao. Ndipo wazo la kuingia katika siasa likanijia, lakini kwa sababu nilikuwa mdogo ilinilazimu kuendelea kwanza na masomo.”

Lakini sasa ameshamaliza masomo na kuanza maisha yake binafsi, Doroth, ambaye ni mtaalamu wa tiba ya viungo, anaweza kutimiza ndoto yake.

“Uchaguzi mkuu ujao nitajitosa katika kinyang’anyiro cha ubunge, lakini ni mapema sana kusema nitagombea jimbo gani kwa sasa,” anadokeza.

“Ila wapenzi wangu wajue tu nitagombea jijini Dar es Salaam.”

Doroth atakuwa akikusanya uzoefu wa kugombea kwa kutumia kazi yake ya ukatibu mkuu, ambayo inamtaka asimamie chaguzi za ndani kwa ngazi zote.

Anasema kazi hiyo ambayo itakijenga chama, pia itasaidia kutengeneza viongozi bora ambao wataiwezesha ACT Wazalendo kupata wagombea wenye sifa kuanzia uchaguzi wa serikali za mitaa mwakani hadi Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Bado kuna watu wenye uwezo

ACT Wazalendo, ambayo kirefu chake ni Alliance for Change and Transparency, ni chama cha kisiasa kilichoanzishwa na kupata usajili wa kudumu 2014 na kinaunganisha nguvu kupigania mabadiliko na uwazi, kikiwa chini ya mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe.

Ni moja ya vyama vya upinzani vilivyoanza kupoteza wanachama wake na viongozi mara tu baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015; baadhi kwa kushindwa katika ubunge au udiwani, wengine kwa kuteuliwa kushika nyadhifa serikalini na wengine kutoona malengo waliyofuata yakitimia.

“Ingawa kuna athari kubwa zimetokea kutokana na wanachama wetu wengi, hasa viongozi wa juu kuondoka, bado kuna watu wenye uwezo wanaoweza kufanya kazi. Mimi naamini chama ni itikadi,” anasema Doroth.

Anasema wanaoondoka upinzani hawatoi sababu za msingi.

“Ikiwa mbunge au diwani anafanya maendeleo katika eneo lake, mwisho wa siku sifa zinakwenda kwa Serikali, hivyo sioni sababu za kuunga mkono juhudi za serikali, badala yake wanapaswa kufanya kazi kwa bidii ili kuwaletea wananchi maendeleo,” anasema kiongozi huyo.

“Kwetu ACT tunajitanabaisha kuwa ni chama cha masuala mbadala na si chama cha mtu. Tunajua Zitto ni kiongozi mkuu ila tukiwa ndani hatuwakwezi watu, ndiyo maana kila mmoja kwa nafasi yake anatakiwa kutimiza wajibu wake.”

Doroth anasema ACT inaamini katika uhuru wa mawazo na mwanachama wao anapoondoka, wao humtakia kheri.

“Lakini mimi sijawahi kuwaza kuondoka ACT,” anasema.

Ingawa amepewa wadhifa huo mkubwa katika utendaji, Doroth anasema wanawake hawaaminiki kama wana uwezo.

Anakumbuka jinsi watu walivyomchukulia siku alipokwenda kwenye msiba mmoja na kukaa eneo ambalo viongozi wa siasa kama mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wa UDP, Gideon Cheyo walikuwa wamekaa.

“Cha kushangaza kabla sijakaa vizuri alinifuata kijana mmoja akaninong’oneza akisema ‘nimeambiwa nikuulize wewe ni nani, maana eneo hili ni maalumu kwa ajili ya viongozi wa siasa’,” anakumbuka.

Na alipomtajia jina na cheo chake katika chama, yule kijana alirejea kwa aliyemuuliza lakini hakutoa maelezo ya kueleweka.

“Amesema sijui na yeye yupo katika siasa,” alimkariri kijana huyo akishangaa jinsi alivyoamua kutotaja cheo alichoelezwa.

“Sijui hakuniamini au alidhani ili kuwa kiongozi lazima uwe mwanamume maana sehemu ile yote nilizungukwa na wanaume tu,” alisema.

“Tanzania tumeshawahi kuwa na wanawake ambao walifika mpaka level (nafasi) ya ukatibu mkuu. Alikuwapo Teddy Kaselabantu na wengineo. Mimi si wa kwanza.”

Doroth anasema ACT Wazalendo hakuna ubaguzi wa aina hiyo kwa kuwa wanaamini katika uwezo na si jinsi.