Daktari azungumzia ugonjwa unaomsumbua Ommy Dimpoz

Ommy Dimpoz 

Muktasari:

Ommy Dimpoz kwa sasa anaendelea na matibabu nchini Afrika Kusini



Dar es Salaam. Wakati supastaa wa muziki wa Bongo Fleva, Ommy Dimpoz akiendelea na matibabu ya koo nchini Afrika Kusini, daktari bingwa wa upasuaji wa magonjwa ya koo, masikio na pua katika Chuo Kikuu cha Afya Shirikishi Muhimbili (Muhas), Godlove Mfuko ameuelezea ugonjwa huo.

Akizungumza na MCL Digital  jana Jumanne Agosti 28, 2018, amesema ugonjwa huo ambao kitaalam unaitwa  ‘Dysphagia’ unaomsumbua mkali huyo wa wimbo wa Yanje,  husababisha mtu kumeza kwa tabu.

Anasema tatizo hilo huanza taratibu kwa mtu kushindwa kumeza chakula au kunywa kimiminika, pia hupata maumivu unapomeza chakula iwapo tatizo hilo limefikiahatua za juu.

“Matatizo yanayosababisha chakula kisipite kutoka kwenye koo kwenda tumboni ni mengi. Yapo ya kuziba kwa umio yaani esophagus na uvimbe wa saratani. Kuna mengine yapo kwenye hypopharynx (sehemu ya chini ya koo ambapo umio linaanzia hapo. Na mengine mengi,” amesema.

Amesema mara nyingi ni uvimbe wa kawaida au saratani lakini amesema kuna vipimo vingi vya kutambua ni ugonjwa upi hasa unaomsumbua mgonjwa.

 Matibabu

Akizungumzia matibabu ya ugonjwa huo, Dk Mfuko amesema kama ni uvimbe wowote umeshakuwa mkubwa pamoja na matibabu yote lazima kunakuwa na huduma ya upasuaji.

“Mwanzoni tunaangalia uvimbe ni wa aina gani, tunafanya kipimo kinachoitwa endoscopy lakini kama hatuwezi kuona vizuri tunafanya  CT Scan ambayo inaweza kuona vizuri zaidi kujua uvimbe umeenda mpaka wapi,” amesema Dk Mfuko.

“Kinyama kidogo hupimwa maabara, kama ni saratani lazima itolewe kwa upasuaji kama ni uvimbe wa kawaida kwenye umio, tunakata ili mtu aendelee kumeza chakula vizuri,” amefafanua Dk Mfuko.

Amesema moja ya matibabu wanayopewa wagonjwa hao ni pamoja na kutoboa tumbo ili chakula kiende moja kwa moja tumboni pasipo kupitia kwenye koo au mdomoni.

 Ukubwa wa tatizo

Dk Mfuko alipoulizwa kuhusu ukubwa wa tatizo hilo hapa nchini alisema hana takwimu halisi, lakini ni tatizo ambalo huwakumba zaidi watu wazima.

“Sina takwimu halisi nimekuwa daktari bingwa kwa miaka mitatu sasa wagonjwa wengi niliokutana nao ni watu wazima niliowaona ni watu kuanzia miaka 50, ngumu kuona mtoto au umri mdogo,” amesema.

Soma Zaidi: