Diwani wa Chadema, Mwenyekiti wapandishwa kizimbani kwa kuharibu kitako cha tenki la maji

Diwani wa Kata ya Segerea (Chadema), Edwin Mwakatobe (37)

Muktasari:

  • Diwani wa Chadema, Edwin Mwakatobe na Mwenyekiti wa Mtaa Serikali ya Mtaa Segerea, Migombani kwa kuharibu kitako cha tenki la maji mnamo Julai 9.

Dar es Salaam. Diwani wa Kata ya Segerea (Chadema), Edwin Mwakatobe (37) amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala kujibu shtaka la kuharibu kitako cha cha tenki la maji chenye thamani ya Sh 830,000.

Mbali na Mwakatobe, mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo ya jinai namba 502 ya mwaka 2018 ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Segerea Migombani, Japhet Kembo (37).

Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali, Ester Kyara amedai leo, Septemba 12, 2018, kuwa washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na shtaka moja la kuharibu mali.

Kyara amedai mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Flora Haule, kuwa washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kutenda kosa hilo Julai 9, 2018 katika Kituo cha daladala cha Segerea kilichopo wilaya ya Ilala.

Kyara amedai siku hiyo ya tukio, katika kituo hicho cha daladala, washtakiwa wanadaiwa kuharibu kitako cha tenki la maji lililojengwa kwa matofali lenye thamani ya Sh 830,000 mali  ya Diana Mbena.

Washtakiwa wamekana shtaka na upande wa mashtaka umedai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika

Hakimu Haule alitaja masharti ya dhamana ambayo ni kuwa na wadhamini wawili kila mmoja, wanaotambuliwa kisheria  watakao saini bondi ya Sh 500,000 kila mmoja.

Hata hivyo, washtakiwa wapo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti.

Hakimu Haule aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 8, mwaka itakapotajwa.