Fastjet yashindwa kutua, Bombardier yashindwa kupaa

Muktasari:

  • Ndege za ATCL zimepachikwa jina ya Bombadier baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kununua ndege mbili kutoka kampuni hiyo ya Canada jambo ambalo limelifanya ATCL ‘kufufuka’ upya.

Mbeya. Wakati ndege ya kampuni ya fastjet ikishindwa kutua jana kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Songwe kutokana na ukungu mzito ulioambatana na mvua, ndege aina ya Bombadier Q400 ya kampuni ya ATCL nayo ilishindwa kuruka kutoka Uwanja wa Ndege wa Mwanza kutokana na hitilafu.

Ndege za ATCL zimepachikwa jina ya Bombadier baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kununua ndege mbili kutoka kampuni hiyo ya Canada jambo ambalo limelifanya ATCL ‘kufufuka’ upya.

Kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Songwe jana, abiria wa fastjet, ambayo imekuwa ikitumia ndege aina ya Airbus A 319 kwa safari za Mbeya, walitarajia kutua Songwe saa 2:00 asubuhi, lakini wakalazimika kurudi Dar es Salaam.

Ndege hiyo ilipofika anga la Mbeya ilikumbana na ukungu ulioambatana na mvua kubwa na kushindwa kutua kwenye uwanja huo ulio kilomita 26 kutoka katikati ya mji.

Kaimu meneja wa uwanja huo, Hamis Amiri alisema marubani wa ndege hiyo waliamua kurudi Dar es Salaam na abiria ili kuepuka hatari ya athari za kufanya majaribio ya kutua.

“Kwanza kulikuwa na mvua kubwa, halafu ukungu pamoja na mawingu vilitanda eneo la uwanja jambo ambalo lilisababisha marubani washindwe kuona vizuri njia ya ndege licha ya kuwapo taa,’’ alisema Amiri.

Tukio la kushindwa kutua kwa ndege hiyo limesababisha abiria waliotarajia kuondoka jana asubuhi kukwama Mbeya huku kampuni ya uwakala wa tiketi za ndege hiyo ikilalamikiwa usumbufu kwa wateja na kampuni.

Wakala mkuu wa fastjet jijini hapa, Erick Sichinga alisema suala la ukungu na mawingu kwenye uwanja wa ndege linahitaji ufumbuzi wa haraka kutokana na kusababisha usumbufu kila mwaka.

Sichinga, ambaye pia ni mkurugenzi mkuu wa Kipunji Heritage Tours and Safari, alisema kwa jana pekee abiria 83 waliotaka kwenda Dar es Salaam walikwama na baadhi walitaka warudishiwe fedha na wengine kuwekwa kwenye hoteli maalumu kupata chai na chakula cha mchana.

“Hali kadhalika kampuni ya fastjet inapata hasara kwani inatumia mafuta ya kuja Mbeya na kurudi na pia inawahudumia abiria katika muda ambao haikutarajia,’’ alisema.

Januari umekuwa mwezi mbaya kwa usafiri wa anga mkoani Mbeya. Januari, 2013 ndege ya fastjet ilishindwa kutua kwenye uwanja huo wa Songwe kutokana na hali ya hewa na mwezi kama huo mwaka jana, ndege ya fastjet ililazimika kurudi Dar es Salaam baada ya kukutana hali mbaya ya hewa.

Wakati hayo yakitokea Mbeya, abiria wa ATCL kwenye Uwanja wa Mwanza juzi wakisubiri kwenda Dar es Salaam, walishindwa kuondoka baada ya ndege yao kushindwa kuruka kutokana na kupata hitilafu.

Akizungumza na gazeti hili mmoja wa abiria hao, Justin Meshack alisema ndege hiyo aina ya Bombadier yenye namba 5H-TCB ilitakiwa kuruka kutoka Mwanza saa 1:00 jioni lakini ilishindwa.

“Mara ya kwanza ndege iliruka baadaye ikatua, ikaruka tena kwa mara ya pili ikatua, ndipo mmoja wa wahudumu akatangaza tushuka ili waikague ndege hiyo kwani ilionyesha kuna tatizo,” alisema Meshack.

Alisema kutokana na tatizo hilo, iliwalazimu kukaa uwanjani hadi saa 6:45 usiku walipochukuliwa na ndege nyingine ya ATCL.

“Tumepata usumbufu sana. Nawaomba (ATCL) wawe wanakagua ndege zao kabla hawajairusha kwa kuwa wakiendekeza uzembe wa namna hiyo, wanahatarisha maisha ya watu,” alisema Meshack.

Abiria mwingine ambaye hakupenda kutaja jina lake alililaumu shirika hilo pamoja na wahudumu wote kushindwa kuikagua ndege hiyo kabla haijaruka.

Akizungumzia tukio hilo, kaimu meneja wa Uwanja wa Ndege Mwanza, David Matovolwa aliomba radhi kwa abiria wote kwa usumbufu waliopata juzi na kwamba ndege hiyo ilishindwa kuruka kutokana na kupata hitilafu lakini alipotakiwa aitaje hitilafu hiyo, hakubainisha.

Alisema kutoka na hitilafu hiyo walifanya mawasiliano na wahusika wa shirika hilo ambao walituma ndege nyingine kutoka Dar es Salaam kuwafuata ambayo ilifika saa 6:45 usiku na walianza safari ya kuelekea Dar es Salaam.

“Abiria walipanda kwenye ndege iliyowafuata na walifika Dar es Salaam saa 7:45 usiku,”alisema Matovolwa.

Matovolwa alisema hizo ni hitilafu za kawaida kwa ndege mpya na kwamba tayari wahandisi kutoka Dar es Salaam ambao walikuja na ndege hiyo, wamefanya matengenezo na iliondoka jana saa 4:00 asubuhi ikiwa haina tatizo lolote.