Fedha za rambirambi zazua balaa kwa katibu CCM

Muktasari:

  • Hata hivyo, Banobi alisema kuna mambo mengi yanapotoshwa na kundi la wanachama waliofunga ofisi na kumtoa nje na kuwa mambo yanayolalamikiwa yameanza kutafutiwa majibu kupitia kanuni na taratibu za chama chao na ukweli utawekwa hadharani.

Baadhi ya wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Kashai wamemtoa nje katibu wa chama hicho, Mikidadi Banobi na kufunga ofisi hiyo kwa madai ya kupokea fedha za rambirambi kutoka kwa Chadema.

Hata hivyo, Banobi alisema kuna mambo mengi yanapotoshwa na kundi la wanachama waliofunga ofisi na kumtoa nje na kuwa mambo yanayolalamikiwa yameanza kutafutiwa majibu kupitia kanuni na taratibu za chama chao na ukweli utawekwa hadharani.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wanachama hao walisema katibu huyo amepokea rambirambi iliyotolewa na madiwani wa Chadema kwenye msiba wa kada wao, Habibu Mahyoro na kwamba wanatakiwa kusomewa mapato na matumizi.

Katibu wa Hamasa wa Vijana Kata ya Kashai, Shaidu Daudi alisema tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki baada ya baadhi ya viongozi wa CCM na wanachama kuchefuliwa na kitendo cha Chadema kutoa rambirambi kwenye msiba wa kada wao ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa kata huku CCM ikikosa kutoa rambirambi.

Alidai chama kilistahili kutoa rambirambi kwa kuwa pamoja na kusimamia miradi pia marehemu alikuwa kada maarufu na mwenyekiti wao.

Mwanachama mwingine ambaye ni mjumbe wa mkutano mkuu wa wilaya, Hazadi Matoke alisema kitendo cha Chadema kutoa rambirambi na wao kukaa kimya kwenye msiba wa kada na kiongozi wao kiliwasononesha wanachama na viongozi walioshiriki maziko huko wilayani Muleba.

Diwani wa Kashai, Nurhulda Kabaju aliyekabidhi rambirambi kwa niaba ya wengine alisema walichukua uamuzi huo ili kuenzi mchango wa Mzee Habibu Mahyoro aliyemtaja kama mpenda demokrasia ambaye hakusita kutoa ushirikiano kwao kwenye masuala yaliyohusu maendeleo ya wananchi.