JPM: Mwacheni Kikwete apumzike

Muktasari:

Hii si mara ya kwanza kuenea kwa habari zinazoonyesha tofauti za viongozi hao na ama Ikulu au Kikwete mwenyewe kujitokeza kuzikanusha.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amewataka watu kuacha kumchonganisha na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete na familia yake na kwamba kiongozi huyo mstaafu aachwe apumzike kwa sababu amefanya kazi kubwa kwa Taifa hili.

Kauli hiyo ya Rais Magufuli imekuja baada ya kuenea kwa taarifa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, kwamba Rais Magufuli anahusika na kuzuiwa mizigo ya mke wa Kikwete, Mama Salma Kikwete kupitia taasisi yake ya Wanawake na Maendeleo (Wama) iliyodaiwa kukwama bandarini kwa madeni ya kodi.

Hii si mara ya kwanza kuenea kwa habari zinazoonyesha tofauti za viongozi hao na ama Ikulu au Kikwete mwenyewe kujitokeza kuzikanusha.

Julai, mwaka huu ulizuka uvumi kwamba Kikwete alikuwa hataki kumkabidhi Rais Magufuli uenyekiti wa CCM.

Hata hivyo, siku ya mkutano mkuu wa CCM mjini Dodoma, Kikwete alisema taarifa hizo hazikuwa za kweli bali yeye ndiye aliyekuwa akimshinikiza Magufuli kuchukua uenyekiti mapema.

Rais Magufuli alithibitisha hilo baada ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti na kumwomba radhi Kikwete kwa kutukanwa kwa sababu yake. Alikiri kupokea simu nyingi za Kikwete akimtaka kuchukua nafasi ya uenyekiti ili aongoze vema.

Oktoba 26 mwaka huu, kauli ya Kikwete aliyoitoa siku ya maadhimisho ya miaka 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) kama Mkuu wa chuo, iliibua utata kwenye mitandao ya kijamii, wengi wakitafsiri kwamba alikuwa akimlenga Rais Magufuli.

Kikwete alisema, “unapokuwa mpya ni lazima watu waone kuna mambo mapya. Lakini mapya ya maendeleo, siyo kubomoa kule tulikotoka.”

Siku iliyofuata baada ya maneno hayo kushika kasi mitandaoni na utata huyo kuripotiwa na vyombo vya habari, Kikwete aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter akisema: “Nimestaafu, naomba niachwe nipumzike. Nisingependa kuhusishwa na siasa za mtandaoni dhidi ya Serikali. Namuunga mkono Rais na Serikali yake.”

“Nasikitishwa sana na matumizi mabaya ya picha zangu mtandaoni hususani watu kunilisha maneno kwa kutaka kutimiza malengo yao ya kisiasa.”

Hata hivyo, Ikulu haikutoa taarifa yoyote baada ya kauli hiyo iliyoibua mijadala kwenye mitandao ya kijamii kwa kuonyesha tofauti za Kikwete na Magufuli.

Rais Kikwete amekuwa akionekana katika shughuli mbalimbali za kitaifa zinazoongozwa na Rais Magufuli, mara ya mwisho alionekana Ikulu kwenye dhifa ya Kitaifa iliyoandaliwa na Rais Magufuli kwa heshima ya Rais wa Zambia, Edgar Lungu.

 

Taarifa ya Ikulu

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Ikulu, Gerson Msigwa, Rais Magufuli amesikitishwa na taarifa hizo ambazo amedai si za kweli na ni uzushi wenye lengo la kumchafua Rais Kikwete.

“Nimesikitishwa sana na uzushi unaofanywa dhidi ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete na mke wake Mama Salma Kikwete. Tafadhali wale mnaotengeneza uzushi huu acheni mara moja na muacheni Rais Mstaafu Kikwete apumzike.”

“Rais Mstaafu Kikwete amefanya kazi kubwa ya kulitumikia Taifa hili, amestaafu anapumzika. narudia muacheni apumzike. Serikali haitaendelea kuvumilia uzushi na uchonganishi huu unaofanywa kwa makusudi ili kuwachafua viongozi wastaafu,” ameonya Rais Magufuli.