Jalada kesi mauaji ya mwanaharakati Wayne Lotter larudishwa polisi

Friday November 22 2019

 

By Hadija Jumanne na Mainda Mhando [email protected]

Dar es Salaam.  Jalada la kesi ya mauaji ya mwanaharakati wa kupambana na ujangili,  Wayne Lotter  inayowakabili washtakiwa 18, wakiwemo raia wawili wa Burundi limerudishwa polisi kwa ajili ya kukamilisha upelelezi.

Wakili wa Serikali mwandamizi, Wankyo Simon ameieleza mahakama hiyo leo Ijumaa Novemba 22, 2019 wakati shauri hilo lilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Amedai jalada hilo baada ya kulipitia walibaini kuwa lina upungufu na  kulirudisha polisi kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho.

Novemba 8, 2019 mahakama hiyo ilielezwa na upande wa mashtaka kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

"Baada ya kufanyiwa kazi mapungufu hayo yaliyojitokeza  jalada  litarudishwa kwetu (ofisi  ya mwendesha mashtaka-DPP) kwa ajili ya kutolewa uamuzi ili tuweze kuandaa nyaraka muhimu za kuihamishia kesi hii mahakama kuu,” amedai Simon.

Wakili huyo amedai kutokana na hali hiyo anaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Advertisement

Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Janeth Mtega ameahirisha kesi hiyo hadi Desemba 6, 2019 huku washtakiwa wakirudishwa rumande  kutokana na kesi ya mauaji kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya mauaji namba 19/2017 ni Nduimana Jonas maarufu mchungaji na Bonimana Nyandwi (raia wa Burundi).

Wengine ni Godfrey Salamba, Inocent Kimaro, Chambie Ally, Robert Mwaipyana,  meneja wa Benki ya Backlays, Khalid Mwinyi; Rahma Almas, Mohammed Maganga, Allan Mafue, Ismail Mohammed, Leornad Makoye, Amino Sha,  Ayoub Selemani, Joseph Lukoa,  Gaudence Matemu, Abuu Mkingie na Abdallah Bawaziri.

Kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kula njama na kumuua Lotter.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, inadaiwa  kati ya Julai Mosi na Agosti 16, 2017 washtakiwa kwa pamoja walikula njama ya kufanya mauaji ya Lotter ambaye alikuwa mkurugenzi mwanzilishi  mwenza wa shirika lisilo la kiserikali la Palms  Foundation.

Siku hiyo katika makutano ya barabara za Chole na Haile Selasie iliyopo wilaya ya Kinondoni  kwa pamoja wanadaiwa kumuua  Lotter.

Advertisement