Jeshi launda bodi kuchunguza ajali iliyoua vijana wa JKT

Vijana wa JKT wa kambi ya Itende Jijini Mbeya wakimsaidia wenzao  wakati wa kutoa heshima za mwisho jana kwa vijana wenzao waliofariki katika ajali iliyotokea Juni 14 mwaka huu eneo la Mwaseka Jijini Mbeya na kusababisha vifo vya watu 13 na majeruhi 48. Picha na Godfrey Kahango.

Muktasari:

Ajali hiyo iliyotokea Juni 14 eneo la Mwasekwa, Mtaa wa Igodima jijini Mbeya, pia ilisababisha vifo vya ofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), dereva na kondakta na kujeruhi vijana wengine 48.

Mbeya. Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Martin Busungu amesema wameunda bodi maalumu kuchunguza chanzo cha ajali iliyoua vijana 10 wa jeshi hilo.

Ajali hiyo iliyotokea Juni 14 eneo la Mwasekwa, Mtaa wa Igodima jijini Mbeya, pia ilisababisha vifo vya ofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), dereva na kondakta na kujeruhi vijana wengine 48.

Vijana hao walikuwa wakisafiri kwenda kambi ya Kikosi cha Jeshi 844 kilichopo Itende jijini Mbeya kwa ajili ya mafunzo ya vitendo wakitokea kambi ya Kikosi cha Jeshi 823 kilichopo Masange JKT mkoani Tabora.

Akizungumza jana wakati wa kuaga miili ya marehemu hao, Meja Jenerali Busungu alisema nguvu kazi ya Taifa imepotea.

“Tayari tumeunda bodi ya uchunguzi ili kujua chanzo halisi cha ajali hiyo ili hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria na utaratibu uliopo,” alisema.

Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali Yakubu Mohammed alisema Taifa limepoteza nguvu kazi kubwa, akitoa mfano wa namna vijana wa JKT walivyotumika kujenga ukuta wa Mirarani mkoani Manyara kuzungumza mgodi wa madini ya Tanzanite.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Florens Turuka alisema sehemu ya jeshi la akiba imepotea lakini pia familia zimepoteza watu muhimu.

Dk Turuka aliwataka vijana walionusurika katika ajali hiyo kutokata tamaa, akisema wizara itaendelea kuwa karibu nao.

Alisema haki na utaratibu unaowahusu waliopoteza maisha na wengine waliopata athari zitafanyiwa kazi kwa haraka.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Paul Ntinika alisema Serikali itaongeza nguvu katika kufanya uchunguzi wa kina ili kupata ukweli wa chanzo halisi cha ajali hiyo.

Hali ya majeruhi

Mkurugenzi wa utumishi wa JKT, Kanali Julius Kadawi alisema hali za majeruhi zinazidi kuimarika na kwamba waliobaki hospitalini ni 15 kati ya 48 waliokuwa wamelazwa katika hospitali tatu.

Alisema waliopo Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya ni saba; Hospitali ya Kanda ya Jeshi-Mbalizi wapo sita na Zahanati ya Kikosi cha JKT-Itende wawili.