Jiji jipya la Dodoma laendelea kutesa wakongwe

Wednesday August 14 2019

Waziri Jafo akizungumza na waandishi kuhusu

Waziri Jafo akizungumza na waandishi kuhusu mapato ya mwaka kwa halmashauri,majiji na mikoa ofisini kwake Mtumba Jijini Dodoma leo 

By Habel Chidawali, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Jiji la Dodoma limeendelea kuwa kinara katika ukusanyaji wa mapato kwa asilimia kubwa huku Mkoa wa Geita ukishika nafasi ya kwanza kwa mikoa.

Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Tamisemi, Seleman Jafo amewaambia waandishi wa habari leo, Agosti 14, 2019 ofisi kwako Mtumba  jijini Dodoma alipokuwa akitoa taarifa ya makusanyo na mapato kwa mwaka 2018/19.

Waziri Jafo amesema lengo la makusanyo yote kwa Majiji 6 ilikuwa ni Sh140.99 bilioni, lakini walikusanya Sh140.48 wakati Dodoma pekee ikikusanya Sh70 bilioni sawa na asilimia 51 ya lengo zima.

Katika orodha ya majiji, Mbeya imeshika nafasi ya mwisho wakati kwa nafasi za mikoa Geita imeongoza kwa kukusanya asilimia 119 na Mtwara imevuta mkia kwa makusanyo ya asilimia 42.

Jafo amesema kiwango cha mapato ya jumla kimeongezeka kutoka asilimia 81 katika mwaka wa fedha 2017/18 hadi kufikia asilimia 91 kwa mwaka wa fedha 2018/19 siri kubwa ikiwa ni matumizi ya mashine za EFD.

Katika hatua nyingine, amesema mwaka huu anatoa zawadi za vinyago kwa waliofanya vibaya kwa halmashauri na mikoa huku akiutaja Mkoa wa Mtwara kuwa utabeba vinyago viwili vya uzembe wakati Geita utapewa ngao kwa kufanya vizuri huku Jiji la Dodoma likitajwa kubeba ngao mbili kwa wakati mmoja ambazo ni makusanyo makubwa na matumizi mazuri katika miradi ya maendeleo.

Advertisement

Advertisement