Jopo la wataalamu lateuliwa kupitia kanuni mpya za Sheria ya Mawasiliano

Muktasari:

  • Pia jopo hilo litapitia na kuchambua vifungu vilivyo kwenye sheria hiyo kuangalia kama vinalinda au kukandamiza uhuru wa habari nchini.

Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa kushirikiana na Muungano wa Taasisi 15 zinazopigania Haki ya Kupata Taarifa (Cori) wameteua jopo la wataalamu kwa ajili ya kupitia kanuni mbili mpya za Sheria ya Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta, kuona kama mapendekezo ya wadau wa habari yalifanyiwa kazi.

Pia jopo hilo litapitia na kuchambua vifungu vilivyo kwenye sheria hiyo kuangalia kama vinalinda au kukandamiza uhuru wa habari nchini.

Katika toleo la Machi 16 la Gazeti la Serikali namba 133 na 134, waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alitangaza kanuni hizo za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Epoka) namba 306 ya mwaka 2010.

Kanuni hizo ni za Sheria ya Mawasiliano na Posta (Maudhui ya Habari za Mitandaoni) ya mwaka 2018 na Sheria ya Mawasiliano ya Kielekroniki na Posta (Maudhui ya Utangazaji katika Redio na Runinga) ya mwaka 2018.

Katika kanuni ya maudhui ya habari za mitandaoni ya mwaka 2018, wachapishaji wa blogu na majukwaa ya mtandaoni wanatakiwa kusajiliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kupata leseni kulingana na gharama zilizoainishwa.

Pia kanuni hiyo inaipa nguvu TCRA kudhibiti mawasiliano ya mtandaoni kwa kuchukua hatua kwa wasiotimiza wajibu ikiwamo kuamuru kuondolewa kwa “maudhui yasiyofaa” na usajili wa watumiaji na majukwaa.

Akizungumza na Mwananchi jana, katibu mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga alisema kazi ya kupitia kanuni hizo itakapokamilika watatoa tamko lao.

“Kwa hiyo kwa sasa sitazungumza lolote mpaka tupate majibu ya wataalamu wanaochambua hizi sheria kuona kama Serikali ilitilia maanani mapendekezo ya wadau, lakini pia kujua kama zinatoa uhuru wa habari na kama hazitoi ni kwanini,” alisema Mukajanga.

Mwenyekiti wa Wamiliki na Waendeshaji wa Mitandao ya Kijamii Tanzania (TBN), Joachim Mushi alisema baada ya kanuni hizo kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali, wamepanga kuonana na mawaziri wenye dhamana ili kujadili jambo hilo.

Alisema wamepanga kuonana na waziri Mwakyembe pamoja na waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa.

“Bado tunaamini Serikali inatujali na hata Rais John Magufuli alivyoingia madarakani aliongea na vyombo vya habari na sisi blogers tukiwepo, kwa hiyo naamini mazungumzo yetu yatapata muafaka,” alisema.

Kanuni hiyo inaeleza kuwa watumiaji wa mitandao watatakiwa kujaza fomu kwa ajili ya kupata leseni kwa gharama ya Sh100,000 na kulipia ada ya Sh1,000,000 kwa muda wa miaka mitatu.

Kwa upande wake, makamu mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, tawi la Tanzania (MISA-Tan), James Marenga alisema kanuni hizo zilizotengenezwa kutokana na kifungu namba 103 (1) cha Sheria ya Udhibiti wa Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya 2010 (Epoca), zina pande mbili.

“Blogers wengi hawana uwezo wa kifedha wa kusajili blogs zao, kwa hiyo wanaweza kuondoka katika sekta hiyo iliyoajiri vijana wengi,” alisema.

Alisema upande wa pili wa kanuni hiyo utasaidia kulinda maadili ya taaluma ya habari kwa sababu watumiaji wa mitandao watapaswa kutafuta upande wa pili wa habari tofauti na sasa ambapo wengi hutumia upande mmoja.

Mmoja wa watumiaji wa mitandao, John John alisema kanuni hiyo ya kufanya usajili wa blogu na majukwaa ya mtandaoni ni kinyume na matakwa ya intaneti inayopatikana bure na kwa uwazi.

“Wamiliki wa blogu wenyewe ambao ni Google hawachaji fedha kuanzisha hizo blogu zao. Sasa kwanini Serikali inataka kutumia fursa hii kujiingizia kipato? Nadhani bado kanuni hii ilipaswa kujadiliwa.” alisema.