Jumaza yaomba msaada Polisi Zanzibar

Muktasari:

Amebainisha kuwa wao kama walinzi wa usalama wa raia na mali zao wanasikitishwa na kupotea kwa viongozi hao na kwamba, wataendelea kushirikiana na familia, ndugu na jamaa ili kujua walipo.


Zanzibar. Baada ya viongozi watano wa dini ya Kiislamu kutoweka katika mazingira ya kutatanisha visiwani Zanzibar, Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (Jumaza) imeviomba vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina juu ya kupotea kwao.

Viongozi hao waliotoweka na maeneo wanayoishi katika mabano ni Amir Haji Khamis Haji (Mpendae), Hamad Ali Haji (Fuoni), Suleiman Juma Suleiman (Makadara), Salum Said Chande (Kinuni) na Abbas Said Chasuma (Kizimbani).

Akizungumza na MCL Digital leo Februari 13, 2018, Naibu Katibu Mtendaji wa Jumaza, Khamis Yussuf Khamis amesema kuwa kupotea kwa watu hao hakuleti taswira nzuri na kuvitaka vyombo kulipa uzito suala hilo na kulifanyia kazi ili kuhakikisha wanapatikana.

Hata hivyo, leo akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Hassan Nassir Ali amesema polisi haina taarifa ya kukamatwa kwa mashehe hao na hawajui walipo.

Amebainisha kuwa wao kama walinzi wa usalama wa raia na mali zao wanasikitishwa na kupotea kwa viongozi hao na kwamba, wataendelea kushirikiana na familia, ndugu na jamaa ili kujua walipo.

Mmoja wa wake wa viongozi hao, Mwanaunguja Abdalla amesema mumewe Haji Khamis Haji aliondoka nyumbani Februari 9, 2018 akielekea msikitini ameshamtafuta maeneo mbalimbali bila mafanikio.