Kaboyoka, Mlinga wavutana tuhuma za ufisadi BoT bungeni

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Naghenjwa Kaboyoka

Muktasari:

  • Mvutano huo unatokana na tuhuma ambazo Mlinga aliziibua Juzi 4, alipokuwa akichangia bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango ya mwaka 2018/19 aliposema BoT kuna ufisadi wa watumishi wake kutumia bima binafsi ya afya badala ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Dodoma. Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Naghenjwa Kaboyoka ameingia katika mvutano na mbunge wa Ulanga (CCM), Goodluck Mlinga kuhusu tuhuma zinazoikabili Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Mvutano huo unatokana na tuhuma ambazo Mlinga aliziibua Juzi 4, alipokuwa akichangia bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango ya mwaka 2018/19 aliposema BoT kuna ufisadi wa watumishi wake kutumia bima binafsi ya afya badala ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Kutokana na tuhuma hizo, Spika Job Ndugai aliiagiza PAC chini ya Kaboyoka kukutana na Mlinga na NHIF na baadaye bodi na menejimenti ya BoT ili kupata ukweli. Pia aliagiza taarifa ifikishwe kwake Juni 11, agizo lililotekelezwa.

Hata hivyo, jana baada ya kipindi cha maswali na majibu kumalizika, Mlinga alisimama akitumia kanuni ya 68(7) kuomba mwongozo wa mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga.

Mlinga alisema kamati zinapoagizwa na spika zifanye kazi zinatakiwa zipeleke ripoti kwa spika ndipo aitolee ufafanuzi.

“Wiki iliyopita (Juni 4) niliongea hapa kuhusu BoT kutumia fedha nyingi kwa ajili ya matibabu kuliko taasisi nyingine za Serikali ambazo zinafanya kazi ngumu. Kamati ya PAC ikakaa na mimi, NHIF na BoT, taarifa nilizonazo hadi sasa bado spika hajalitolea majibu suala hilo,” alisema Mlinga.

“Lakini (juzi) jana nimeona kwenye taarifa ya habari mwenyekiti wa kamati ya PAC (Kaboyoko) akitoa taarifa za kamati ambayo ni siri mpaka spika atakapotolea majibu, akisema taarifa kuhusu BoT kutumia fedha nyingi kwenye matibabu si za kweli.”

“Nilikuwa nataka nielekezwe kuhusu utaratibu kwa sababu hata mimi nina mengi ya kuongea kuhusu hilo, lakini nimeheshimu kiti na kunyamaza mpaka pale spika atakapolitolea majibu maana hata kwenye kamati yenyewe nilizongwazongwa kwa sababu ya kugusa masilahi ya watu.”

Mbunge huyo aliomba aelekezwe kuhusu utaratibu na kama anaruhusiwa kwenda kuongea na vyombo vya habari kwa kuwa akifanya hivyo kuna watu watakimbia ofisi zao.

Mwenyekiti wa Bunge, Najma alisema suala hilo ni kinyume cha kanuni na spika atalishughulikia.

Alimtaka Mlinga kutozungumza na vyombo vya habari kwa kuwa akifanya hivyo atakuwa amekiuka kanuni za Bunge na atachukuliwa hatua.

Kaboyoka ambaye ni mbunge wa Same Mashariki (Chadema) alipotafutwa na Mwananchi nje ya viwanja vya Bunge kuhusu alichosema Mlinga bungeni, alisema, “Hakuna sehemu niliposema BoT wametumia fedha nyingi au kidogo na hakuna kanuni niliyovunja labda anatafuta umaarufu tu.”