Kalapina, Mwakalebela kukimbilia mahakamani

Aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo la Kinondoni kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, Karama Masoud ‘Kalapina’.

Muktasari:

Mwakalebela alidai jana kuwa katika Jimbo la Iringa Mjini kulikuwa na dosari za kukusanya na kutangaza matokeo.

Dar es Salaam. Waliokuwa wagombea ubunge katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika nchini hivi karibuni, Frederick Mwakalebela (Iringa Mjini-CCM) na Karama Masoud ‘Kalapina’ (Kinondoni ACT- Wazalendo) wamesema wanatarajia kwenda mahakamani kupinga matokeo.

Mwakalebela alidai jana kuwa katika Jimbo la Iringa Mjini kulikuwa na dosari za kukusanya na kutangaza matokeo.

Naye Kalapina alidai kuwa matokeo ya Kinondoni ni batili, endapo uamuzi wa mahakama utaonyesha kuwa ameshindwa kihalali ataridhika. “Sikutendewa haki na mkurugenzi wa uchaguzi na mawakala wa vyama vingine ambao waliwatisha mawakala wangu,” alisema.

Hata hivyo, msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Vallence Urassa alikana madai hayo akisema ni uongo.

Kalapina alisema anawasiliana na mwanasheria wake, Edward Mwakingwe wanajadili ajenda za kupeleka mahakamani, hadi kufikia wiki ijayo,” alisema.

Alisema mawakala wake walikuwa wakitishiwa kupigwa na mawakala wa Chadema na CUF jambo alilosema lilisababisha ashindwe katika uchaguzi huo.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Magdalena Sekaya alisema: “Malalamiko hayo siyo ya kweli, kwanini asiandike barua kwetu ili tumjibu badala ya kulalamika kwenye vyombo vya habari.”

Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene alisema anashangazwa na mgombea huyo kulalamikia mawakala wa Chadema kutoa vitisho kwa mawakala wake badala ya kulalamikia masuala ya msingi yaliyoharibu uchaguzi mzima.

Mshindi wa ubunge Jimbo la Kinondoni ni Maulid Said Mtulia (CUF) alipata kura 70,337 baada ya kumshinda Idd Azzan (CCM) aliyepata kura 65,964.