Kalemani afukua ‘kaburi’ la miaka minne Mkuranga

Wednesday August 8 2018

 

By Bakari Kiango, Mwananchi [email protected]

Mkuranga. Ni miaka minne sasa tangu wakazi wa vijiji 17 vya kata tatu za jimbo la Mkuranga wafungiwe miundombinu ya umeme, lakini mpaka leo hawana huduma hiyo.

Katika kata hizo za Mbezi, Ndondo na Kisiju miundombinu hiyo iliwekwa tangu 2014.

Wakitoa malalamiko yaliyojaa historia ya mradi huo jana mbele ya Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani, wakazi wa maeneo hayo walisema kukosekana kwa umeme kunawakosesha ajira vijana wa eneo hilo.

“Hapa kuna viwanda vinne kikiwamo cha kusindika dagaa kamba na kutengeneza boti za kisasa ambavyo vyote vimefungwa,” alisema Ramadhan Hamis, mkazi wa eneo hilo.

Mkazi mwingine, Maulid Mwinyimkuu alieleza kuwa wanalazimika kwenda Mkuranga mjini kufuata huduma ya kuchaji simu.

“Hali yetu ni mbaya na tunakosa maendeleo kwa kwa sababu ya umeme. Tulikubali minazi na miembe yetu ikatwe kupisha umeme lakini hatuoni matunda yake,” alisema.

Hata hivyo, Dk Kalemani aliuvunja mzizi wa fitina na kuliagiza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuhakikisha umeme unawaka ndani ya siku 14.

“Hii haingii akilini yaani nguzo zipo lakini umeme hakuna. Nawaomba watendaji wa Tanesco waje mbele yenu,” alisema.

Baada ya kuwaita watendaji hao, Dk Kalemani alisema makosa yalifanyika kwa Tanesco kumuachia mkandarasi MBH aliyekuwa akitekeleza awamu ya pili ya Wakala wa Umeme Vijijini (Rea) bila kukamilisha kazi hiyo.

“Mmewaona hawa watendaji (anawaonyesha kwa kidole) ndiyo watakaosimamia mradi huu hadi ukamilike, nawapa siku 14 kuanzia kesho (leo) nataka kazi ianze,” alisema.

Pia, aliwataka watendaji kutafuta mafundi popote walipo kwa ajili ya kuanza kazi ili wakazi wa vijiji hivyo wapate nishati hiyo waliyoikosa kwa muda mrefu.

Naye mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ulega alisema inasikitisha kuona watu wanajitolea maeneo yao, lakini wanakosa huduma kwa muda mrefu.

Advertisement