Kamishna Idara ya Kazi amchefua Majaliwa TIC

Wednesday December 5 2018

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Wajumbe wa Bodi ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), alipotembelea kituo hicho jijini Dar es salaam, jana. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu 

By Elizabeth Edward, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka watendaji wa Serikali kuondoa mazingira ya urasimu yanayosababisha kukwama kwa shughuli za uwekezaji.

Majaliwa alitoa agizo hilo jana alipotembelea Kituo cha Taifa cha Uwekezaji (TIC) ikiwa ni mara ya kwanza tangu kihamishiwe chini ya ofisi yake kutoka Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Pamoja na kuzungumza na wakurugenzi na watendaji wa kituo hicho, Majaliwa alitembelea kituo cha pamoja cha utoaji huduma kinachokusanya idara zote za Serikali.

Akiwa kwenye kituo hicho alipata taarifa za kusimama kwa mfumo wa utoaji vibali vya kazi kwa kile kilichodaiwa kuwa Kamishna wa Kazi, Gabriel Malata bado anajifunza kuhusu mfumo huo.

“Haiwezekani kazi ishindwe kufanyika kwa sababu ya mtu mmoja, anajifunza wapi? Kwa muda gani na inakuwaje shughuli zisimame, inatakiwa kazi ziendelee wakati anaendelea kujifunza,” alisema Waziri Mkuu.

Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Godfrey Mwambe aliomba yafanyike marekebisho ili kuondoa ukinzani wa sheria zinazoratibu utendaji kazi wa idara na taasisi za Serikali zinazohusika na uwekezaji.

Alisema uwapo wa ukinzani wa kisheria wakati mwingine unaleta mkanganyiko kwa wawekezaji na kusababisha ugumu katika kutambua ni hatua zipi anazotakiwa kuzifuata mwekezaji kwa mtiririko unaofaa. Hivi karibuni Rais John Magufuli alikihamishia Kituo cha Taifa cha Uwekezaji katika ofisi ya Waziri Mkuu ili utendaji wake uwe chi ya uratibu wa ofisi hiyo.

Advertisement