Kesi ya 'Mpemba wa Magufuli' yashindwa kuendelea kutokana na shahidi kupata dharura

Wednesday August 14 2019

 

By Fortune Francis, Mwananchi. [email protected]

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeshindwa kusikiliza ushahidi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili, Yusuf Ali Yusuf, maarufu  ‘Mpemba wa Magufuli’ kutokana na shahidi kupata dharura.

Yusuf na wenzake watano, wanakabiliwa na mashtaka manne ikiwemo kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh785.6milioni.

Leo, Agosti 14,2019 , Wakili wa Serikali Candid Nasua, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba amedai kuwa kesi hiyo imekuja kwaajili ya kusikilizwa lakini upande wa mashtaka hawana shahidi.

Hakimu Simba amedai Wakili wa Serikali Mkuu Nchimbi alikuja na kusema hawana shahidi kutokana na kupata dharura hivyo kesho sitataka kusikia hakuna shahidi.

"Mwambie Nchimbi kile alichokisema nimefikisha ujumbe  alionifikishia nimeufikisha kama ulivyo kwa washtakiwa na mawakili wao hivyo kesho shahidi atakuwepo" ameeleza Hakimu Simba

Baada ya maelezo hayo Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 15  itakapoendelea na ushahidi.

Advertisement

Washtakiwa wote wamerudishwa rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili kutokuwa na dhamana.

Mbali na Yusuph (35), washtakiwa wengine katika kesi hiyo  ni Charles Mrutu (37), maarufu kama mangi mapikipiki na mkazi wa Mlimba, Morogoro; Benedict Kungwa (40), mkazi wa Mbagala Chamazi;  Jumanne Chima (30), maarufu kama JK na mkazi wa Mbezi;  Ahmed Nyagongo (33), dereva na mkazi wa Vikindu-Mkuranga na Pius Kulagwa (46)mfanyabiashara na mkazi wa Temeke.

 

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka manne, likiwemo la kujihusisha na mtandao wa ujangili, katika kesi ya uhujumu uchumi namba 53/2016.

Miongoni mwa shtaka kati ya mashtaka manne yanayowakabili washtakiwa hao ni  kwamba, kati ya Januari, 2014 na Oktoba, 2016, katika maeneo ya Jiji la Dar es Salaam, Tanga, Iringa na Mtwara, walijihusisha na mtandao wa ujangili kwa kukusanya na kuuza nyara za Serikali ambazo ni vipande 50 vya meno ya tembo vyenye thamani ya dola za Marekani 180,000 sawa na Sh392 milioni bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Advertisement