Kesi ya Halima Mdee yakwama tena

Muktasari:

Halima Mdee anakabiliwa na kesi hiyo akidaiwa kutoa maneno ya uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli Julai 3, 2017 katika Makao Makuu ya Ofisi ya Chadema iliyopo mtaa wa Ufipa wilaya ya Kinondoni .

Dar es Salaam. Ushahidi wa kesi inayomkabili mbunge wa Kawe, Halima Mdee haukusikilizwa leo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya mshtakiwa (Mdee) katika kesi hiyo kudaiwa anaumwa.

Hayo yameelezwa leo Septemba 11 na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Akizungumza mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, Mutalemwa amesema kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa leo Septemba 11 kwa mashahidi wa upande wa mashtaka kutoa ushahidi lakini mshtakiwa hayupo akidaiwa kuumwa

Baada ya Kishenyi kueleza hayo, mdhamini wa Halima Mdee, Fares Robinson aliieleza mahakama kuwa anaumwa.

Hakimu Simba baada ya kusikiliza Maelezo ya upande hizo zote aliipanga kesi hiyo kusikilizwa tena Oktoba 8, mwaka huu ambapo mashahidi wa upande wa mashtaka wataendelea kutoa ushahidi wao.

Katika kesi hiyo mashahidi wawili wa upande wa mashtaka tayari wamekwishatoa ushahidi wao ambao ni Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Ilala(RCO),  Davis Msangi na Mkuu wa Kituo cha polisi cha Urafiki,Mrakibu wa Polisi Batseba  Kasanga.

Mdee alifikishwa mahakamani hapo kwa Mara ya kwanza Julai 10, mwaka huu.